Afrika Kusini, China zafanya warsha kuhusu tiba ya jadi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 27, 2021

CAPE TOWN - Warsha ya siku nne yenye lengo la kuimarisha mawasiliano kati ya sekta ya tiba ya jadi ya Kiafrika na China kwa ajili ya uvumbuzi imeanza Jumatatu ya wiki hii mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Warsha hiyo inayoandaliwa kwa pamoja na Ubalozi wa China nchini Afrika Kusini, mamlaka ya usimamizi wa Tiba ya jadi ya China na Chuo Kikuu cha Western Cape, imehusisha mada mbalimbali zikiwemo kuunda mfumo na uvumbuzi, kufanya utekelezaji na kutoa mafunzo, matumizi na udhibiti wa mitishamba asilia, utafiti wa kupunguza umaskini na janga la UVIKO-19.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Aunkh Chabalala ambaye ni mkurugenzi wa uvumbuzi wa teknolojia inayotegemea maarifa asilia katika Idara ya Sayansi ya Afrika Kusini amesema, Afrika Kusini na China zina ushirikiano wa muda mrefu katika tiba ya jadi, na nchi hizo mbili zina ushirikiano mzuri katika sekta hiyo kupitia ushirikiano wa utafiti kati ya vyuo vikuu vya nchi hizo mbili.

"Tutajifunza mengi kutoka kwa wataalamu wa China, pia tutaangalia ni mambo gani tunaweza kujifunza ili kufikia malengo yetu (ya kujumuisha tiba ya jadi katika mfumo wa afya wa kitaifa)" Bruce Mbedzi, mkurugenzi wa tiba ya jadi katika Idara ya Afya ya Afrika Kusini, amesema wakati wa ufunguzi.

Kwa mujibu wa konsela wa Ubalozi wa China nchini Afrika Kusini Shen Long, warsha hiyo siyo tu itaongeza uelewa wa madaktari wa Afrika Kusini kuhusu tiba ya jadi ya China, lakini pia itakuza ushirikiano katika sekta ya tiba ya jadi kati ya China na Afrika Kusini katika siku zijazo.

Kwa upande wake, Zhu Haidong, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika mamlaka ya usimamizi wa Tiba ya jadi ya China amesema anatumai warsha hiyo itaongeza uelewa wa dawa za mitishamba za Afrika na dawa za mitishamba za China kwa lengo la kuchangia afya ya watu nchini Afrika Kusini.

Warsha hiyo itafuatiwa na kongamano la tiba ya jadi la Afrika Kusini na China, litakaloratibiwa na Idara ya Sayansi na Ubunifu ya Afrika Kusini na mamlaka ya usimamizi wa Tiba ya jadi ya China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha