

Lugha Nyingine
Uchumi wa Afrika Mashariki kuongezeka kwa asilimia 4.1 Mwaka 2021: AfDB
NAIROBI, Kenya – Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekadiria kwamba uchumi wa ukanda wa Afrika Mashariki unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.1 Mwaka 2021, kutoka asilimia 0.4 Mwaka 2020,
Kwa mujibu wa Mtazamo wa Kiuchumi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Mwaka 2021 uliotolewa Alhamisi ya wiki hii na benki hiyo, uchumi wa kanda hiyo utaimarishwa kutokana na kuendelea kufufuka kwa uchumi wa dunia.
"Hata hivyo, utoaji hafifu wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 na hatari za kuongezeka kwa maambukizi zinaweza kupunguza makadirio hayo. Janga hili limekuwa na athari mbalimbali katika kanda nzima, huku nchi zinazotegemea sana utalii zaidi zikiwa zimeathiriwa zaidi," Benki hiyo imesema.
Ripoti hiyo inapitia hali ya uchumi wa nchi zikiwemo Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Tanzania na Uganda.
Mtazamo wa uchumi wa kikanda wa Mwaka 2021 unachambua ukuaji wa uchumi, vichochezi vyake, na athari za matokeo ya kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na umaskini, ajira, na ukosefu wa usawa wa mapato, kwa kuzingatia athari za janga la UVIKO-19.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kanda ya Afrika Mashariki ina unyumbufu wa kiuchumi, na ndio kanda pekee barani Afrika ulioepuka kudidimia kwa uchumi Mwaka 2020.
AfDB inahusisha unyumbufu wa uchumi wa kanda ya Afrika Mashariki kwa mwaka jana wakati wa janga la UVIKO-19 na hali ya anuwai ya uchumi na utekelezaji wa haraka wa sera zilizochukuliwa na serikali ili kukabiliana na athari za janga hilo.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa Afrika Mashariki inatarajiwa kuimarika uchumi kuanzia mwaka 2021 hadi kufikia katikati ya karne hii.
Benki hiyo ya Afrika imependekeza haja ya kuwa na sera za uratibu wa uchumi ili kuharakisha ufufukaji wa uchumi wa kanda hiyo na kujenga uthabiti baada ya janga la UVIKO-19. Benki hiyo pia inapendekeza kuongeza kasi ya utoaji chanjo na kubuni na kutekeleza bajeti ya kuchochea uchumi na mikakati ya ufufukaji wa uchumi ili kufikia miradi ya kuaminika ya uchumi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma