

Lugha Nyingine
Bei ya mafuta duniani yapanda wakati wafanyabiashara wakisubiri mkutano wa OPEC+
NEW YORK - Bei ya mafuta duniani imepanda Jumatatu ya wiki hii huku wafanyabiashara wakisubiri mkutano muhimu wa OPEC+ utakaokutanisha kwa pamoja Shirika la Nchi Zinazouza Petroli na washirika wake.
Kampuni ya West Texas Intermediate katika mauzo yake ya Desemba imeongeza senti 48 ili kupata dola za kimarekani 84.05 kwa pipa kwenye Soko la Biashara la hisa la New York. Bei ya mafuta ghafi yanayosafirishwa mwezi Januari kutoka kampuni ya Brent imeongezeka senti 99 hadi kufikia dola za kimarekani 84.71 kwa pipa kwenye Soko la ICE la London.
Nchi wanachama wa OPEC+ wanatarajiwa kukutana siku ya Alhamisi ya wiki hii, kujadili mpango wake kuhusu uzalishaji wa mafuta ghafi. Kundi hilo la nchi zinazozalisha mafuta linapunguza hatua kwa hatua upungufu wa uzalishaji mafuta uliofanywa mwaka jana.
Carsten Fritsch, mchambuzi wa nishati katika Taasisi ya Utafiti ya Commerzbank ya Ujerumani, amesema Jumatatu kwenye taarifa kwamba, "Kuna mashaka" kama OPEC+ itaongeza uzalishaji wake wa mafuta kwa kiwango kikubwa au la.
"Kauli zilizotolewa na nchi mbili za jumuiya hiyo, Saudi Arabia na Urusi, zinaonesha kuwa uzalishaji mwezi Desemba utaongezeka kama ilivyopangwa kwa mapipa 400,000 kwa siku. Wanachama wengine wawili wakubwa wa jumuiya hiyo, Iraq na Kuwait hivi karibuni wametoa kauli zinazofanana." ameongeza.
Katika wiki iliyopita, kiwango cha bei ya mafuta ghafi cha Marekani kilipungua kwa asilimia 0.2, huku bei ya mafuta ya Brent ikipungua kwa asilimia 1.3.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma