Makala: Ushirikiano wa kilimo kati ya China na Tanzania wasaidia wakulima kuondokana na umaskini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 18, 2021

DAR ES SALAAM - Fikiri Kisairo, mkulima wa kijiji cha Kitete wilayani Kilosa mkoani Morogoro, anatembea kwa maringo wakati akitembelea shamba lake la mahindi yaliyostawi.

"Siku zangu za kukosa usingizi usiku nikifikiria jinsi ya kupata ada kwa watoto wangu wawili wanaosoma shuleni zimepita" anasema Kisairo, mmoja wa wanufaika wa ushirikiano wa kilimo kati ya China na Tanzania ambao umedumu kwa miaka 10, na kuwaondoa mamia ya wakulima wa Tanzania kutoka kwenye umaskini.

Mwaka 2019 Kisairo alijiunga na mradi wa kilimo cha mahindi unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Tanzania katika vijiji kadhaa mkoani Morogoro ili kupunguza umaskini miongoni mwa wanavijiji.

Mkulima huyo ambaye Jumanne ya wiki hii alishiriki kwenye kongamano la Mafanikio ya mradi wa Ushirikiano wa Kilimo kati ya China na Tanzania: Teknolojia Ndogo, Mavuno Makubwa, amesema alijiunga na mradi huo wa mahindi baada ya kutimiza masharti ya mkulima wa mfano wa kuigwa na kushiriki katika mradi huo kwa miaka mitatu.

“Kuongezeka kwa mavuno ya mahindi kuliniwezesha kuondokana na umaskini kwani sasa nina chakula cha kutosha na ninauza ziada ya mahindi ili kujiongezea kipato” amesema kwenye jukwaa hilo mkoani Morogoro, takriban umbali wa kilomita 200 Magharibi mwa Mji Mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.

Kisairo mwenye familia ya watu watano alijisifu kuwa kwa sasa anafanikiwa kuwalipia ada ya shule watoto wake wawili na amechimba kisima kirefu cha maji ambacho anakitumia kumwagilia bustani yake ya mbogamboga yenye ukubwa wa hekta 1.21 kwa mwaka mzima ikiwemo majira ya kiangazi.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela, amesema kuwa kwa msaada wa mamlaka za mkoa huo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China, wakulima wanaojiunga na mradi huo wameongeza uzalishaji wa mahindi, na wakulima wa mfano wa kuigwa 1,667 wamelima angalau ekari moja (karibu hekta 0.4) ya mahindi kila mmoja.

Kongamano hilo pia lilishuhudia uzinduzi wa mradi mpya unaojulikana kwa jina la "Uboreshaji wa mnyororo wa thamani wa maharage ya soya mkoani Morogoro" utakaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China kuanzia Mwaka 2021 hadi 2022.

“Huu ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,” amesema Shigela.

Shigela amesema, kama mradi wa majaribio, wakulima wa mfano wa kuigwa 200 katika vijiji vinne watashirikishwa na kupewa mafunzo ya uzalishaji, usindikaji na uuzaji wa soya na bidhaa za soya kama vile maziwa ya soya na unga wa soya. "Mradi huu unalenga kuboresha hali ya afya ya wanakijiji pamoja na kuongeza mapato yao."

Ulaji wa soya ni miongoni mwa hatua kuu za uingiliaji kati kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa kukuza uzalishaji wa soya na kuanzisha uongezaji thamani wa soya na matumizi kwa mahitaji ya lishe ya jamii.

Xu Chen, Balozi mdogo wa China nchini Tanzania, amesema katika suala la ushirikiano wa kilimo, China na Tanzania ni washirika wazuri.

Amesema kuwa mradi wa mahindi siyo tu unakuza uzalishaji wa mahindi, bali pia unaboresha hali ya maisha ya wakulima wengi kwa kushiriki uwekezaji wa China katika sekta ya kilimo nchini Tanzania. Ameongeza kuwa mazao mengi zaidi ya kilimo ya Tanzania yanaingia katika soko la China.

Kwa upande wake, Denis Nkala, Mratibu wa Kanda ya Asia na Pasifiki wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Ushirikiano wa Kusini-Kusini (UNOSSC), amesema, mfano mmoja wa ushirikiano kati ya China na Afrika kwa ajili ya utoshelevu na usalama wa chakula, unaofuata mtazamo utokanao na mahitaji na wadau mbalimbali, ni mradi huo wa Teknolojia Ndogo, Mavuno Makubwa, ambao unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China nchini Tanzania.

“Kupitia kubadilishana mbinu bora za kulima, mradi unalenga kuongeza uzalishaji wa mahindi mara tatu, kuongeza mapato ya wakulima, hatimaye kuchangia katika kupunguza umaskini, usalama wa chakula na kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu nchini Tanzania,” amesema Nkala. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha