Maonesho ya bidhaa ya Shandong yafunguliwa Nairobi huku uhusiano wa Kenya na China ukiimarika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 18, 2021

NAIROBI –Katika kusaidia kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya China na Kenya, Maonesho ya Nne ya Bidhaa zinazouzwa Nje ya Shandong yamefunguliwa katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi.

Zhang Yijun, Balozi mdogo wa China nchini Kenya amesema katika ufunguzi wa maonesho hayo Jumatano ya wiki hii kuwa, maonyesho hayo ya siku tatu yatatoa jukwaa pana la kuonesha viwanda na mashine ya China yenye kiwango cha juu kwa kampuni za Kenya.

"Maonesho hayo pia yataimarisha njia yenye ustawi wa muda mrefu itakayoleta mustakabali mzuri wa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya China na Kenya," Zhang amesema.

Kwa mujibu wa Afripeak Expo Kenya ambao ni waratibu wa maonesho hayo, ujumla kampuni 103 zinashiriki katika maonesho hayo, na kampuni 83 kati yao zinatoka nje ya Kenya hususan China.

Maonesho hayo yatafanyika kwa njia ya mtandaoni na nje ya mtandaoni ambapo mashine za kisasa za kilimo kutoka China, mashine za ujenzi, vifaa na zana, bidhaa za nishati ya jua na nishati mpya, vipuri vya magari, bidhaa za kemikali na vifaa vya matibabu vitaoneshwa.

Akizungumzia uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na China, Zhang amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya Mwaka 2021, thamani ya jumla ya biashara kati ya China na Kenya iliongezeka kwa asilimia 29.9 hadi kufikia Shilingi za Kenya Bilioni 560 (sawa na Dola Bilioni 5 za Marekani) licha ya janga la UVIKO-19.

Ameongeza kuwa, mwaka jana wa 2020, uwekezaji wa moja kwa moja wa China nchini Kenya ulifikia Dola za kimarekani Milioni 172 na thamani ya kandarasi mpya zilizotiwa saini baina ya pande hizo mbili ilifikia Dola za kimarekani Bilioni 3.2.

Gao Wei, Mkurugenzi Mtendaji wa Afripeak Expo Kenya, amesema kuwa janga la UVIKO-19 limeathiri uchumi wa Dunia, na ili kukuza viwanda vya ndani, maonesho hayo yameweka banda la Kenya ambalo litatoa fursa kwa kampuni 20 za Kenya kuonesha bidhaa zao na kuunganishwa na wanunuzi wa China.

Kwa upande wake, Erick Rutto, naibu mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda nchini Kenya (KNCCI), amesema kuwa, maonesho hayo ni jukwaa mwafaka la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya China na Afrika.

"Ni ishara muhimu kwa dunia kwamba China inafungua mlango licha ya kuongezeka kwa wimbi la kujilinda kibiashara" ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha