EAC yakaribia kukamilisha mfumo wa ushuru ili kuendana na AfCFTA

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 18, 2021

DAR ES SALAAM - Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imepiga hatua muhimu kuelekea kukidhi mahitaji ya biashara chini ya Eneo la Biashara huria la Bara la Afrika (AfCFTA), huku ikiendelea kukamilisha mfumo wa ushuru wa EAC.

Taarifa iliyotolewa Jumatano wiki hii kwenye Makao Makuu ya EAC mjini Arusha na Baraza la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI), imeiagiza sekretarieti ya EAC kuitisha vikao na wataalam ifikapo Desemba 15, 2021, ili kukamilisha viwango vipya vya ushuru wa EAC,

Taarifa hiyo inasema sekretarieti ya EAC iliagizwa kufanya tathmini ya idadi ya tozo za ziada ambazo zimetolewa na kila nchi mwanachama kutoka aina mbalimbali.

Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki, amesema kuwa kazi nyingi zinahitajika kufanywa ili kuanzisha biashara chini ya makubaliano ya AfCFTA.

"Jumuiya za kiuchumi za kikanda ni nyenzo kuu katika utekelezaji wa AfCFTA. EAC inapenda kutekeleza sera, maamuzi na maagizo, ili kurahisisha biashara chini ya makubaliano yaliyowekwa kwa ajili ya kupanua ushirikiano na kuongeza biashara barani Afrika," amesema.

Nchi za Afrika zilianza biashara rasmi chini ya AfCFTA Januari 1, 2021, ambayo yanaunganisha watu Bilioni 1.3 kote barani Afrika. Nchi wanachama wa EAC ni Burundi, Kenya, Sudan Kusini, Rwanda, Tanzania na Uganda. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha