Uzalishaji wa umeme wa Tanzania wapungua kwa 345MW kutokana na kina cha maji katika mabwawa kupungua

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 19, 2021

DAR ES SALAAM – Shirika la Ugavi wa Umeme la Tanzania (TANESCO) limetangaza kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa umeme hali inayosababishwa na kupungua kwa kina cha maji katika mito na mabwawa ya kuzalisha umeme.

Katika taarifa yake kwa umma Alhamisi wiki hii, TANESCO imesema kwamba uzalishaji wa umeme kwa siku umepungua kwa Megawati 345 (MW), kiwango ambacho ni sawa na asilimia 21 ya uzalishaji wa umeme kwa siku.

Taarifa hiyo haikutaja kiwango cha umeme kinachozalishwa kila siku lakini imehusisha kupungua kwa uzalishaji wa umeme na kushuka kwa kiwango cha maji katika mito na mabwawa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uzalishaji wa umeme umeathirika vibaya katika mitambo ya TANESCO ya Kihansi, Pangani na Kidatu.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema TANESCO imechukua hatua za haraka za kuzalisha umeme kupitia mitambo yake kwa kutumia gesi asilia.

“Utaratibu huu ulitarajiwa kuzalisha jumla ya Megawati 358,” inasema taarifa hiyo na kuongeza kuwa baadhi ya mikoa itakuwa na tatizo la kukatika kwa umeme kwa muda maalum. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha