Wakati Jumuiya ya Kimataifa ikipongeza muafaka Sudan, Mkuu wa Majeshi aiomba AU kuirejeshea Sudan Uanachama

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 22, 2021

KHARTOUM - Karibu mwezi mmoja tangu mgogoro wa kisiasa kuzuka nchini Sudan, Jenerali Mkuu wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan na Waziri Mkuu aliyeondolewa Abdalla Hamdok Jumapili ya wiki iliyopita wametia saini azimio la kisiasa ambalo ni pamoja na kumteua tena Hamdok kuwa waziri mkuu.

Azimio hilo limebainisha kuwa waraka wa kikatiba ndiyo utakuwa udhamini mkuu katika kipindi cha mpito. Pia limehakikisha ushiriki mpana wa kisiasa, isipokuwa kwa chama kilichovunjwa cha National Congress Party cha Rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir.

Azimio hilo linasisitiza kwamba ushirikiano kati ya vitengo vya kiraia na kijeshi ndiyo utaleta uhakika wa uthabiti na usalama wa Sudan, na kulipa Baraza Kuu jukumu la kusimamia kipindi cha mpito bila kuingilia kazi za serikali.

Pia makubaliano hayo yametoa ahadi ya kuchunguza vifo na kujeruhiwa kwa raia na wanajeshi wakati wa maandamano ya hivi karibuni na kukamilisha taasisi za mpito, ikiwa ni pamoja na bunge na mahakama.

Katika hafla ya kutia saini azimio hilo iliyorushwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa ya Sudan, Hamdok amesema kutiwa saini kwa azimio hilo kunafungua milango kwa masuala yote ya mpito.

“Kuna changamoto kubwa zinazoikabili hali halisi ya kisiasa, lakini tuna uwezo wa kufanya kazi pamoja,” amesema.

Kwa upande wake Al-Burhan, amesema azimio hilo "linaweka misingi sahihi ya kipindi cha mpito kwa njia ya maafikiano."

Hatua hiyo ya muafaka wa Sudan, imepongezwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmed Aboul-Gheit kwa nyakati tofauti wametoa taarifa za kupongeza maendeleo hayo mazuri ya kisiasa nchini Sudan.

Sambamba na makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan Abdel Fattah Al-Burhan Jumapili iliyopita ametoa wito kwa Umoja wa Afrika kurejesha uanachama wa Sudan katika Umoja huo.

Sudan imekuwa ikikumbwa na mgogoro wa kisiasa baada ya Al-Burhan kutangaza hali ya dharura Oktoba 25 mwaka huu na kuvunja Baraza Kuu na Baraza la Mawaziri. Mnamo Novemba 11, Al-Burhan alitoa amri ya kikatiba ya kuamuru kuundwa kwa Baraza Kuu la mpito, na akajitaja kama mwenyekiti wa baraza hilo. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha