Uhusiano kati ya China na Afrika waimarika licha ya changamoto za UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 24, 2021

KAMPALA, Uganda - Mawaziri wa Afrika na wenzao wa China watakutana nchini Senegal baadaye mwezi huu kwa ajili ya Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Mawaziri hao watakusanyika wakati Dunia bado inapambana na janga la UVIKO-19 ambalo kwa mujibu wa wataalam wa uchumi, limeharibu uchumi wa nchi nyingi, hasusan za Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kiuchumi.

Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne ya wiki hii kuhusu mkutano ujao uliopangwa kufanyika Novemba 29-30, mwaka huu amesema kuwa changamoto kama vile UVIKO-19 zimethibitisha uhusiano kati ya China na Afrika na kuufanya uimarike zaidi.

"Mshikamano na ushirikiano ndiyo silaha zenye nguvu zaidi za kushinda UVIKO-19, na mwanga wa ushirikiano hakika utaondoa ukungu wa janga hili," mwanadiplomasia huyo wa China amenukuliwa akisema. "Tangu kuzuka kwa janga hili, kwa mujibu wa mahitaji ya Afrika, China imetoa msaada wa haraka wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa, chanjo na timu za wataalam kwa nchi 53 za Afrika na Umoja wa Afrika."

Zhang amesema, uhusiano huo madhubuti utasaidia nchi za Afrika kufungua na kufufua tena uchumi wao.

Mawaziri hao watakapokutana Dakar, Mji Mkuu wa Senegal, watapanga na kupata jibu la pamoja kuhusu UVIKO-19 na pia mwelekeo wa uhusiano kati ya China na Afrika katika miaka mitatu ijayo na baadaye.

Pembezoni mwa mkutano huo wa mawaziri, unaotarajiwa kuwa na kaulimbiu ya "Kuimarisha Ushirikiano kati ya China na Afrika na Kukuza Maendeleo Endelevu ili Kujenga Jumuiya ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja katika Enzi Mpya," Mkutano wa Saba wa Biashara kati ya China na Afrika pia utafanyika

"Tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2000, FOCAC imezingatia kanuni ya mashauriano ya kina, michango ya pamoja na manufaa ya pamoja, na kuwa jukwaa linalojumuisha usawa, vitendo na ufanisi," Zhang amesema juu ya Baraza hili la ushirikiano ambalo sasa limefikisha miaka 21. "FOCAC imeongoza ushirikiano wa kimataifa na Afrika na kuwa chapa maarufu kwa ushirikiano wa Kusini-Kusini."

Kwa mujibu wa takwimu za Ubalozi wa China nchini Uganda, tangu kuanzishwa kwa FOCAC, biashara kati ya China na Afrika na uwekezaji wa China barani Afrika umeongezeka kwa mara 20 na 100. China imejenga na inaendelea kujenga katika nchi mbalimbali za Afrika reli zaidi ya Kilomita 10,000, barabara karibu Kilomita 10,000, miradi ya kuzalisha umeme yenye Megawati 120,000 na mkongo wa mtandao wa intaneti wenye urefu wa Kilomita 150 .

China pia imejenga zaidi ya vituo 400 vya matibabu, taasisi za elimu zaidi ya 1,200, na uwezo wa kuzalisha tani 400,000 za maji safi na salama kwa kila mwaka. Katika miaka iliyopita, nafasi za ajira zaidi ya milioni 4.5 zimepatikana barani Afrika kutokana na ushirikiano huo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha