Mjumbe Mkuu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Libya ajiuzulu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 24, 2021

UMOJA WA MATAIFA- Mjumbe Mkuu Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Libya, Jan Kubis amejiuzulu, mwezi mmoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi muhimu katika nchi hiyo.

"Naweza kuthibitisha kuwa Bw. Kubis amewasilisha barua ya kujiuzulu kwake na katibu mkuu amekubali kwa masikitiko," amesema Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumanne ya wiki hii.

"Katibu Mkuu anatafuta mtu mbadala anayefaa kuchukua nafasi yake. Sote tunafahamu kikamilifu ajenda ya uchaguzi na tunafanya kazi haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha uendelevu wa uongozi," Dujarric amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika New York Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Msemaji huyo bila kueleza ni kwa muda gani Kubisi atasalia katika nafasi yake, alisema kwamba Kubis hataacha kazi yake mara moja na anatarajiwa kutoa taarifa kwa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Libya siku ya leo ya Jumatano.

"Niongeze pia kwamba tuna uwepo imara nchini Libya na wenzetu wote wataendelea na kazi kama walivyofanya, kushirikiana na mashirika ya Libya kwa kuzingatia uchaguzi ujao, bila kusahau changamoto za kibinadamu ambazo watu wa Libya wanakumbana nazo" Dujarric amenukuliwa akisema.

Bila kutoa maelezo ya ziada, Dujarric amesema kuwa kujiuzulu kwa Kubis hakukuja kwa mshangao kwa katibu mkuu, na kwamba hakuna kutoelewana kati yao kulikosababisha kujiuzulu kwa Kubis.

Nafasi hiyo ya Mjumbe Maalum iliundwa kwa azimio Na. 2542 la Baraza la Usalama la Septemba Mwaka 2020. Azimio hilo linagawanya kazi ya awali ya uongozi wa mwakilishi maalum kuwa mbili: mjumbe maalum ambaye anaongoza kwa ujumla Tume ya Msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) ambaye pia anazingatia hasa ofisi ya upatanishi wa wahusika wa mgogoro wa Libya na washirika wa kimataifa ili kumaliza mzozo, na mratibu anayesimamia shughuli za kila siku na usimamizi wa UNSMIL.

Mjumbe huyo maalum yuko Geneva na mratibu yuko Libya.

Hadi wakati wa kupitishwa kwa Azimio hilo Na. 2542, nafasi ya uongozi wa UNSMIL ilikuwa wazi kwa muda wa miezi sita kufuatia Ghassan Salame kujiuzulu ghafla kuwa mjumbe maalum wa Libya.

Pendekezo la Guterres la kumteua mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa wa mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, kuwa mjumbe maalum wa Libya lilipata uungwaji mkono wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama katikati ya mwezi Desemba Mwaka 2020.

Hata hivyo, wiki iliyofuata baada ya kuteuliwa, Mladenov alitangaza kujiuzulu kufanya kazi na Umoja wa Mataifa bila kutarajiwa, hivyo kumfanya kupoteza sifa za kuhudumu kwenye nafasi hiyo mpya.

Mnamo Januari Mwaka huu wa 2021 Guterres alimteua Kubis kutoka Slovakia kuwa mjumbe wake maalum kwa Libya hadi sasa anapojiuzulu nafasi hiyo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha