China yapinga vikali Marekani kualika mamlaka ya Taiwan kuhudhuria "Mkutano wa kilele wa Demokrasia"

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2021

Beijing - China imeeleza kupinga vikali mwaliko wa Marekani kwa mamlaka ya Taiwan kushiriki katika kile kinachoitwa mkutano wa kilele wa demokrasia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amesema Jumatano ya wiki kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kualika Taiwan kwenye kile kinachoitwa mkutano wa kilele wa demokrasia.

Zhao amesema kuwa kuna uwepo kwa China moja tu duniani, na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ndiyo serikali pekee halali inayowakilisha China. Taiwan ni sehemu isiyotengeka ya China, na Sera ya kuwepo kwa China moja ndiyo inayotambulika duniani kote na ndiyo inayoongoza uhusiano wa kimataifa. Taiwan haina hadhi katika sheria za kimataifa isipokuwa hadhi yake ikiwa sehemu ya nchi ya China.

"Tunaitaka Marekani kuzingatia kanuni ya kuwepo kwa China moja na mambo husika ya makubaliano matatu ya pamoja kati ya China na Marekani, na tunaitaka Marekani iache kutoa jukwaa lolote au kuunga makundi ya 'ufarakanishaji wa Taiwan", Zhao amesema, huku akiongeza kuwa kucheza na moto linapokuja suala la "ufarakanishaji wa Taiwan" hatimaye kutaibua moto kwa Marekani yenyewe.

Kuhusu kile kinachoitwa mkutano wa kilele wa demokrasia, Zhao amesema kuwa China imeweka wazi msimamo wake mara nyingi.

Zhao amesema kuwa, demokrasia ni thamani ya pamoja ya watu wote, na haiwezi kumilikiwa na nchi chache. Kile ambacho Marekani imefanya kinathibitisha kwamba demokrasia ni kisingizio tu na chombo kinachotumiwa na Marekani kuendeleza malengo yake ya kijiografia, kukandamiza nchi nyingine, kuifarakanisha Dunia na kutumikia maslahi yake binafsi.

Ameongeza kuwa, Marekani inafuata siasa za makundi na kuchochea mapigano kwa kisingizio cha demokrasia, ambayo inaibua mawazo ya Vita Baridi na kuibua upinzani wa jumuiya ya kimataifa.

Sambamba na China, Russia nayo kupitia Msemaji wa Kremlin imeeleza kwamba mkutano huo wa kilele wa demokrasia ulioitishwa na Marekani unalenga kuzitenganisha nchi na Dunia katika vipande hasa kutokana na kualikwa kwa Taiwan na kuachwa kwa nchi nyingine kwenye mkutano husika.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema orodha ya waalikwa, iliyotolewa Jumanne kwenye tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, inaonesha kuwa Washington "inaunda njia mpya za kugawanya, kugawanya nchi katika kile ambacho- kwa maoni yao - ni nzuri, na zile mbaya."

"Nchi nyingi zaidi zinapendelea kujiamulia namna ya kuishi," Peskov amewaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa Washington "inajaribu kubinafsisha neno 'demokrasia'."

Marekani imealika nchi kadhaa kwenye mkutano huo uliopewa jina la "Mkutano wa kilele wa Demokrasia", zikiwemo washirika wake wakuu wa Magharibi. Mkutano huo uliotangazwa kwa muda mrefu utafanyika mtandaoni Tarehe 9 na 10 Desemba mwaka huu kabla ya mkutano wa ana kwa ana katika mkutano wake wa pili mwaka ujao.  

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha