Ripoti yaonesha Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” linabadilisha maendeleo ya Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2021

NAIROBI - Pendelezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” (BRI), lililotolewa na Rais Xi Jinping wa China miaka minane iliyopita, linabadilisha maendeleo ya Kenya kwa kiwango kikubwa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Sera ya Afrika Jumatano ya wiki hii, tangu pendekezo la BRI kutolewa Mwaka 2013, China imetoa msaada katika miradi ya kisasa ya miundombinu nchini Kenya kama vile reli, barabara, bandari, mabwawa, viwanda, mawasiliano ya kidijitali ambayo yameleta uhai kwa ukuaji wa uchumi wa Kenya.

"Katika muongo uliopita, Kenya imejenga reli mpya kabisa ya kisasa ya Kilomita 670 ya Standard Gauge (SGR) inayounganisha Bandari ya Mombasa na Bandari kavu ya Naivasha," inasema katika ripoti hiyo iliyopewa jina la "Mafanikio ya Pamoja: Kufuatilia Utekelezaji wa Ukanda Mmoja na Njia Moja nchini Kenya, 2018-2021."

Ripoti hiyo ilichunguza mchango halisi za BRI kupitia miradi mahususi katika maeneo matano ambayo ni ujenzi wa miundombinu, mashauriano ya sera, ukuzaji wa biashara, ushirikiano wa kifedha na maingiliano kati ya watu na watu nchini Kenya.

Hadi sasa BRI imesaidia miradi kama vile ujenzi wa barabara, reli na bandari zinazovuka na kuunganisha nchi 172.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, SGR ya Kenya iliyojengwa kwa msaada wa China ina handaki la pili kwa ukubwa barani Afrika ambalo kipekee limekuwa ni kivutio cha watalii.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa kutokana na BRI, Kenya imeshuhudia ongezeko kubwa la viwanda vipya vinavyoajiri maelfu ya watu na kukuza uchumi.

Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian amesema wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kuwa, China na Kenya ni marafiki wazuri, washirika wazuri na ndugu wazuri.

"Ushirikiano wetu wa kivitendo wenye mafanikio mengi unaonekana wazi katika ushirikiano kati ya China na Afrika," amesema Balozi Zhou, huku akibainisha kuwa China itashirikiana bega kwa bega na Kenya ili kuendeleza ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na kutekeleza matokeo ya Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ili kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi zote mbili.

Kwa upande wake Kirimi Kaberia, Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Biashara, amesema “BRI pia imeboresha muunganisho wa Bara la Afrika, kuondoa vizuizi vya mipaka na kuhimiza biashara ndani ya bara hilo."

Ameongeza kuwa, katika miaka siyozidi kumi ya uundaji na utekelezaji wa BRI, Kenya sasa ina bandari mpya ya kina kirefu katika mji wa pwani wa Lamu, SGR ambayo imebadilisha usafirishaji wa bidhaa, pamoja na maelfu ya kilomita za barabara ambazo zimebadilisha uchukuzi katika kanda hiyo. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha