Ripoti ya UN yaonesha janga la UVIKO-19 limeongeza ukatili dhidi ya wanawake

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2021

UMOJA WA MATAIFA - Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) iliyoangazia athari za UVIKO-19 kwa usalama wa wanawake nyumbani na katika maeneo ya umma inaonesha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Jumatano wiki hii yenye kichwa “Kupima kivuli cha janga: Unyanyasaji dhidi ya wanawake wakati wa UVIKO-19", takriban nusu ya wanawake waliripoti kwamba wao au mwanamke wanayemfahamu walikumbwa na aina fulani ya ukatili tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19.

Ripoti hiyo ambayo msingi wake ni takwimu kutoka nchi 13, inaonesha kuwa takriban robo ya wanawake hawajihisi salama nyumbani huku migogoro iliyopo ikiongezeka ndani ya kaya tangu janga hili lianze.

Ripoti hiyo iliyotolewa katika mkesha wa Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake, ambayo inaangukia Novemba 25 inaeleza kwamba, wanawake walipoulizwa kwa nini walihisi kutokuwa salama nyumbani, walitaja unyanyasaji wa kimwili kuwa mojawapo ya sababu (asilimia 21). Baadhi ya wanawake walisema kwamba waliumizwa na wanafamilia wengine (asilimia 21) au kwamba wanawake wengine nyumbani kwao walikuwa wakiumizwa (asilimia 19).

Wakiwa nje ya nyumbani kwao, wanawake pia walikuwa wakihisi kuathiriwa zaidi na unyanyasaji, huku asilimia 40 ya waliohojiwa wakisema hawahisi salama wakati wakitembea peke yao usiku tangu kuanza kwa UVIKO-19. Takriban wanawake 3 kati ya 5 pia walidhani kwamba unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya umma ulizidi wakati wa UVIKO-19.

"Ukatili dhidi ya wanawake ni janga lililopo la kimataifa ambalo hustawi katika majanga mengine. Migogoro, maaafa ya maumbile yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa chakula na ukiukwaji wa haki za binadamu, yote hayo yanachangia wanawake na wasichana kuishi katika hali ya hatari, hata katika nyumba zao, vitongoji au jamii,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake Sima Bahous katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa mabadiliko ya sera ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Guterres alisema, ukatili dhidi ya wanawake unaepukika. Sera na miradi inayofaa huleta matokeo, hiyo ina maana ya mikakati ya kina na ya muda mrefu ambayo inakabiliana na sababu kuu za unyanyasaji, kulinda haki za wanawake na wasichana, na kukuza harakati za kudai haki za wanawake.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha