Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Sweden ajiuzulu saa chache baada ya kuchaguliwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 25, 2021

Picha kutoka maktaba iliyopigwa Agosti 26, 2021 ikimuonesha Magdalena Andersson Kiongozi wa Chama cha Social Democrat kwenye mkutano na waandishi wa habari huko Stockholm, Sweden. Muda mfupi baada ya kuchaguliwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke, Madgalena Andersson Jumatano ya Novemba 24, 2021, aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwake huku akikabiliwa na changamoto kubwa ya kuongoza serikali ya mseto ya walio wachache. (Magnus Liljegren/Regeringskansliet/Kwa mkono kupitia Xinhua)

STOCKHOLM - Muda mfupi baada ya Kiongozi wa Chama cha Social Democrat Magdalena Andersson kuchaguliwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Sweden siku ya Jumatano ya wiki hii, ameandika barua ya kuomba kujiuzulu huku akikabiliwa na changamoto kubwa ya kuongoza serikali ya mseto ya walio wachache.

Saa chache tu baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu, Bunge la Sweden (Riksdag) lilipitisha pendekezo la bajeti lililowasilishwa na vyama vya upinzani na kusababisha mshirika wa muungano wa chama anachokiongoza Andersson, Green Party kuondoa uungaji mkono wake. Hatua hii ilimlazimu Andersson kutangaza kujiuzulu kwake.

Mwenendo wa matukio hayo ya Jumatano ulitokana na matokeo ya uchaguzi wa Mwaka 2018 ambayo hayakuamua mshindi wa jumla kuweza kuunda Serikali hivyo kusababisha mchakato mrefu wa kisiasa wa kuunda serikali ambapo vyama fulani hufanya kila liwezalo kuzuia wapinzani wao wa kiitikadi kupata ushawishi wa aina yoyote.

Wachambuzi wanasema uchaguzi wa Andersson ulikuwa kama upepo. Kwani ili kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu, alihitaji tu wabunge wengi katika Bunge la Riksdag lenye jumla ya viti 349 kumpigia kura. Katika uchaguzi huo wa Jumatano aliungwa mkono na wabunge 117 huku akikataliwa na 174, na wengine 57 waliacha kupiga kura. Mbunge mmoja hakuwepo.

Kuchaguliwa kwa Andersson kuwa Waziri Mkuu kulitokana na makubaliano ya saa 11 na Chama cha Mrengo wa Kushoto, ambacho kiliweka sharti la kuongezwa kwa pensheni kwa wastaafu wapatao 700,000 maskini ili kumuunga mkono.

Hata hivyo, baadaye siku hiyo pendekezo la bajeti ya muungano wa vyama vinavyotawala wa Social Democrat na Green Party lilikataliwa na wabunge huku wakiunga mkono bajeti iliyopendekezwa kwa pamoja na muungano wa vyama vitatu vya upinzani ambavyo ni cha Mrengo wa Wastani, Sweden Democrats na Christian Democrats.

Haya yanajiri baada ya chama cha Mrengo wa Kati, ambacho kilimkubali Andersson kama waziri mkuu katika jaribio la kukiangusha Chama cha Swedish Democrats chenye sera ya kupinga wahamiaji, kuamua kutopigia kura pendekezo la bajeti ya serikali.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha