Kampuni ya TECNO ya China yaliteka soko la Afrika kwa suluhu zilizoboreshwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 26, 2021
Kampuni ya TECNO ya China yaliteka soko la Afrika kwa suluhu zilizoboreshwa
Muuzaji akimuonesha mteja simu mahiri ya Tecno kutoka Kampuni ya China ya Transsion Holdings mjini Nairobi, Kenya. (Picha/Xinhua)

Kampuni ya China ya Transsion Holdings ambayo ina chapa tatu za simu za TECNO, itel na Infinix, imekuwa miongoni mwa chapa maarufu za simu barani Afrika kutokana na suluhu zake zilizoboreshwa kwa watumiaji.

Kampuni hiyo ya kutengeneza simu za kisasa yenye makao makuu yake mjini Shenzhen, China ilitunukiwa tuzo ya bingwa wa kitaifa wa utengenezaji bidhaa mnamo Novemba 15 kwa teknolojia yake ya kamera iliyobuniwa kwa ajili ya soko la Afrika na masoko mengine.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Kimataifa la Ushauri la IDC, Kampuni ya Transsion ilishika nafasi ya kwanza kwa kuchukua sehemu kubwa ya soko barani Afrika mwaka jana, na iliendelea na mwelekeo mzuri mwaka huu wa 2021.

Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, kampuni ilipata mapato ya yuan bilioni 35.77 (sawa na dola bilioni 5.6 za kimarekani) katika robo tatu za kwanza za mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 43.26 kwa mwaka. Faida halisi katika kipindi hicho iliongezeka kwa asilimia 47.79 hadi yuan bilioni 2.88.

Ripoti hiyo ya kampuni kwa kipindi cha katikati ya Mwaka 2021 inaeleza zaidi kwamba, ukiacha ubunifu wa kamera kwa ajili ya watumiaji wa Afrika, Kampuni ya Transsion pia inaendeleza mradi wake wa akili bandia kwenye sauti ili kukabiliana vyema na lafudhi mbalimbali za wenyeji na kutumia algoriti kupunguza kelele ya chinichini.

Kuanzia Afrika na sasa kulenga kupanua biashara zake katika maeneo mengine duniani, Kampuni ya Transsion imeendelea kujenga mtandao wake wa usambazaji barani Afrika. Tarehe 20 Oktoba, ilitia saini makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya KAF katika eneo huru la biashara la Djibouti kwa ajili ya ukuzaji wa huduma za usambazaji.

Kampuni hiyo imesema, eneo hilo huru la biashara la Djibouti litaunganisha vituo vingine vya kimataifa vya usafirishaji kama vile Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Djibouti na Reli ya Addis Ababa-Djibouti ili kuhudumia zaidi masoko ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha