Uchumi wa China watarajiwa kukua kwa asilimia 5.3 Mwaka 2022

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 08, 2021
Uchumi wa China watarajiwa kukua kwa asilimia 5.3 Mwaka 2022
Mfanyakazi akifanya kazi kwenye karakana ya utengenezaji wa vitambaa ya kampuni moja ya vitambaa vyenye teknolojia mpya katika wilaya ya Fucheng, Hengshui, Mkoa wa Hebei, Kaskazini mwa China, Novemba 30, 2021. [Picha/Xinhua]

Akademia ya Sayansi ya Jamii ya China (CASS) imeeleza kwamba uchumi wa nchi hiyo unatarajiwa kuongezeka kwa karibu asilimia 5.3 Mwaka 2022 kufuatia ongezeko linalotarajiwa la asilimia 8 mwaka huu.

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na akademia hiyo kuhusu makadirio ya uchumi wa China, watunga sera wanapaswa kuweka lengo la ongezeko la uchumi la Mwaka 2022 zaidi ya asilimia 5, ili kuwapa nafasi zaidi ya kukabiliana na changamoto na kuzingatia kusukuma mageuzi na kuimarisha maendeleo ya kiwango cha juu.

Li Xuesong, Mkurugenzi wa Taasisi ya uchumi wa kiasi na kiteknolojia chini ya CASS ameeleza kwamba, mbinu kama vile kupunguza au kuongeza kiwango cha riba na uwekezaji wa miundombinu husisitiza hatua ndogo lakini za haraka za kufikia malengo ya muda mrefu kutegemea kama uchumi uliopo sasa unashuka au unaongezeka.

"Sera ya fedha ya China inahitaji kuendelea kuchukua hatua za haraka Mwaka 2022, kwa kuzingatia kuongeza ufanisi na ubora wake, hasa katika nyanja kama vile uboreshaji wa viwanda na ukuzaji wa miji," Li alisema kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Beijing, Mji Mkuu wa China. "Na sera imara ya fedha inapaswa kuzingatia kuleta utulivu wa ongezeko la mikopo na kukabiliana na mfumuko wa bei."

Li amebainisha kwamba, kwa kukabiliana na hali mbaya na ngumu ya kiuchumi ndani na nje ya nchi, serikali inapaswa kutilia maanani katika kuhakikisha utulivu wa bei na utoaji wa kutosha wa bidhaa, kuimarisha mnyororo wa uzalishaji na ugavi, kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19, kuendelea kuhimiza uvumbuzi wa teknolojia , kupanua ipasavyo mahitaji ya ndani, kujiandaa kukabiliana na hatari na kupanua mageuzi na kufungua mlango katika sekta muhimu.

Waraka huo unasema ongezeko la asilimia 5.3 la Mwaka 2022 linalotarajiwa litaufanya wastani wa makadirio ya ongezeko la uchumi kwa mwaka katika kipindi cha 2020-2022 kufikia asilimia 5.2, juu ya asilimia 5.1 kutoka Mwaka 2020 hadi 2021.

Waraka huo unakadiria kwamba bei ya jumla ya bidhaa nchini China itapanda kiasi Mwaka 2022, na kiwango cha bei cha wazalishaji na kiwango cha bei cha watumiaji vikiongezeka kwa asilimia 5 na asilimia 2.5. Na thamani ya uagizaji wa bidhaa na uuzaji bidhaa kwa nje katika Mwaka 2022 inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 10.4 na asilimia 6.

"Tunatarajia sera ya uchumi wa jumla italegezwa ili kukabiliana na shinikizo la kushuka kwa ongezeko la uchumi," Louis Kuijs, mkuu wa uchumi wa Asia katika Taasisi ya utafiti wa uchumi ya Oxford.

"Tunafikiri watunga sera wana maamuzi ya mwisho kuhusu ongezeko la Pato la Taifa GDP, ambao kwa sasa huenda ni karibu asilimia 5 kwa mwaka... Kwa makadirio yetu ongezeko la GDP litashuka hadi asilimia 3.6 katika robo ya nne ya mwaka huu, tunakadiria watunga sera watachukua hatua zaidi ili kukuza ongezeko la uchumi mwishoni mwa Mwaka 2021 na mapema ya Mwaka 2022."

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha