Taasisi ya Confucius yaingiza uhai katika uhusiano kati ya China na Namibia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 15, 2021

WINDHOEK - Vijana wa Namibia wanaojifunza lugha ya Kichina katika Taasisi ya Confucius kwenye Chuo Kikuu cha Namibia huongeza ujuzi wao wa lugha walioupata ili kuchangamkia fursa.

Grace Nande mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na kozi ya lugha ya Kichina katika Taasisi hiyo Mwaka 2016. Nande, ambaye kwa sasa yuko mwaka wake wa nne wa masomo katika chuo kikuu, akihimizwa na bibi yake, ambaye alisafiri kwenda China, kwa maslahi binafsi na udadisi vikiwa sababu ya mwelekeo wake wa kuendelea na kozi ya lugha ya Kichina.

Kutokana na kujifunza lugha ya Kichina, leo anapata fursa ambazo hapo awali hakufikiria kuzipata.

Mwaka 2017, alikuwa mmoja wa wanafunzi waliochaguliwa na Taasisi ya Confucius kushiriki katika Kambi ya Majira ya joto huko Beijing, China. Hadi kufikia Mwaka 2019, jumla ya wanafunzi 90 walishiriki katika mpango wa kambi ya majira ya joto.

Kwa mujibu wa Nande, hii ilikuwa fursa nzuri ya kubadilishana ujuzi wa lugha na kufahamu utamaduni na historia ya kale ya China, kutembelea maeneo kama vile Ukuta Mkuu na Uwanja wa Tian'anmen.

"Pia nilitembelea sehemu ya kisasa ya Beijing ikiwa ni pamoja na teknolojia ya kiwango cha juu, Ukumbi wa Kitaifa wa Michezo ya Kuigiza na Makao Makuu ya Taasisi ya Confucius. Sikuwahi kuwa na ndoto kwamba ningetembelea China, kujifunza lugha ya Kichina kumewezesha hilo," Nande amesema katika mahojiano ya Jumatatu ya wiki hii.

Soin Ndalimbililwa alianza kujifunza lugha ya Kichina Mwaka 2017 akiwa kidato cha pili (shule ya sekondari). Mwaka huo huo, alishiriki katika Mashindano ya Daraja la Lugha ya Kichina kwa wanafunzi wa shule za sekondari na akapata nafasi ya kwanza.

"Kujipatia fursa ya kushiriki mashindano ya kimataifa nchini China ni mafanikio yangu makubwa zaidi. Mpango wangu wa baadaye ni siku moja kutengeneza application (app) itakayotafsiri lugha yangu ya asili kwenda Kichina ili kupunguza kikwazo cha lugha," Ndalimbililwa anasema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Namibia, Liu Dianbo, amesema fursa ya kujifunza lugha ya Kichina imepokelewa vyema nchini Namibia, na kuwavutia zaidi ya raia 5,900 wa Namibia ambao wamejifunza kozi ya Kichina tangu kufunguliwa kwa Taasisi hiyo Mwaka 2013.

Kwa mujibu wa Liu, kando na jukumu la kufundisha, Taasisi hiyo pia inakuza uhusiano kati ya China na Namibia kwa kubadilishana utamaduni na fursa nyingine zinazopatikana.

"Hakika, kujifunza lugha ya Kichina kwa wenyeji kunarahisisha kutoa fursa, kujenga zaidi uwezo wa wenyeji, na kuchangia maendeleo ya kitaifa kupitia Taasisi ya Confucius," Liu amesema.

Dk. Marius Kudumo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Namibia amesema kuwa kujifunza lugha ya Kichina nchini Namibia ni ufunguo wa kujenga uhusiano imara kati ya Namibia na China na kukuza uhusiano wa kiutamaduni.

"Hatimaye, imeongeza maelewano, kutoa faida nyingi na kuongeza nguvu za ushindani kwa vijana wa Namibia," Kudumo amesema.

Taasisi ya Confucius imeanzisha maeneo 15 ya kufundishia Lugha ya Kichina huko Windhoek na miji ya Ongwediva, Rundu, Walvis Bay, na Swakopmund. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha