

Lugha Nyingine
Moderna yasema chanjo yake ya nyongeza ya UVIKO-19 yaonesha ufanisi dhidi ya Omicron
Mfanyakazi wa afya aliyevaa barakoa akitayarisha dozi ya chanjo katika kituo cha chanjo huko Los Angeles, California, Marekani, Desemba 15, 2021. (Xinhua)
WASHINGTON - Kampuni ya baioteknolojia ya Marekani Moderna imetangaza kuwa data za awali zinaonesha kwamba dozi yake ya nyongeza ya chanjo ya UVIKO-19 inaonekana kuongeza kiwango cha kingamwili dhidi ya kirusi kipya cha korona aina ya Omicron.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo mapema Jumatatu ya wiki hii inaeleza kwamba, dozi ya nyongeza ya chanjo ya Moderna iliyoidhinishwa ya mikrogram 50 dhidi ya UVIKO-19 mRNA-1273 iliongeza mara 37 ya kiwango cha kingamwili dhidi ya Omicron ikilinganishwa na kiwango cha kabla ya dozi ya nyongeza, na dozi ya nyongeza ya mikrogram 100 iliongeza mara 83 ya kiwango cha kingamwili.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, dozi ya nyongeza ya mikrogram 100 ilikuwa "salama kwa ujumla na ilivumiliwa vyema," Hata hivyo, kampuni hiyo imesema kwamba kulikuwa na athari mbaya za mara kwa mara kufuatia kudungwa dozi ya nyongeza ya mikrogram 100 ikilinganishwa na dozi ya nyongeza ya mikrogram 50.
Stephane Bancel, Afisa Mtendaji Mkuu wa Moderna amesema, ili kukabiliana na kirusi cha korona aina ya Omicron kinachoambukiza zaidi, Moderna itaendelea kuharakisha utafiti wa chanjo mbadala wa dozi ya nyongeza dhidi ya Omicron katika jaribio la kliniki ikiwa itahitajika katika siku zijazo.
Kirusi cha korona aina ya Omicron, ambacho kina uwezo wa kuambukiza zaidi kuliko kile cha Delta, kilikuwa kimepatikana katika angalau majimbo 47 ya Marekani hadi kufikia Jumapili, tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa nchini humo huko California mnamo Desemba 1 mwaka huu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma