Rais wa CAF asema AFCON haitaahirishwa tena

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 23, 2021

YAOUNDE - Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe amesema kuwa Mashindano ya Kombe la Afrika (AFCON), yaliyopangwa kufanyika mwakani nchini Cameroon, yataendelea kama ilivyopangwa, na kumaliza uvumi ulioenea kwamba mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili yanaweza kuahirishwa tena kutokana na UVIKO-19.

"Nitakuwa hapa Januari 7 (Mwaka 2022) na nitakuja kutazama soka," Motsepe amewaambia waandishi wa habari baada ya kukutana na Rais wa Cameroon Paul Biya, mjini Yaounde, Mji Mkuu wa Cameroon, Jumanne wiki hii.

Amesema CAF itahakikisha mashindano hayo ya AFCON hayashuhudii maambukizi ya UVIKO-19.

"Hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia uwanjani bila kipimo cha PCR (kipimo cha virusi vya korona). Itabidi tuwalinde mashabiki" Motsepe amesema.

"Ni kweli, kutakuwa na wasiwasi juu ya matokeo feki ya vipimo, lakini tunashughulikia masuala hayo. Tunapaswa kuwa na imani na kujiamini sisi wenyewe kama Waafrika. Na tunapaswa kuwa na imani kwamba tunaweza kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Cameroon," amesema.

Awali michuano hiyo ilipangwa kufanyika Juni na Julai Mwaka 2021 lakini CAF ilitangaza Januari 15, 2020, kwamba kutokana na hali mbaya ya hewa katika kipindi hiki, michuano hiyo itafanyika kuanzia Januari 9 hadi Februari 6, 2021. Juni 30, 2020, CAF iliahirisha tena mashindano hayo kwa mara ya pili hadi Januari Mwaka 2022 kutokana na janga la UVIKO-19.

Siku ya Jumatatu wiki hii, Motsepe alitembelea Uwanja wa Olembe mjini Yaounde, ambao unaendelea kujengwa. Uwanja huo utakuwa mwenyeji wa ufunguzi na ufungwaji wa michezo hiyo.

AFCON imepangwa kuanza nchini Cameroon Januari 9 Mwaka 2022 na kuendelea kwa wiki nne katika viwanja sita tofauti nchini humo.

Kutokana na mlipuko wa janga la korona, baadhi ya wafuatiliaji wa soka la Afrika walianza kujadili uwezekano wa kuahirishwa tena kwa mashindano hayo. Siku za hivi karibuni klabu za soka za Ulaya zenye wachezaji wa Afrika ambao watashiriki michuano hiyo zimeonesha wasiwasi wa afya ya wachezaji wao huku kukiwa na dalili za kuzuia wachezaji kushiriki kutokana na hofu ya kuambukizwa UVIKO-19.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha