China yathibitisha maafisa wa Marekani kutuma maombi ya viza ya kuhudhuria Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 28, 2021

Mwenge wa Olimpiki wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing ya Mwaka 2022 ukioneshwa kwa umma katika Bustani ya Shougang huko Beijing, Mji Mkuu wa China, Desemba 13, 2021. (Xinhua/Zhang Chenlin)

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amethibitisha kuwa China imepokea maombi ya viza kutoka kwa wafanyakazi husika wa Marekani ya kuhudhuria Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing.

Msemaji Zhao amethibitisha hilo katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu ya wiki hii, alipotakiwa kuzungumzia ripoti hizo zilizosema hivi karibuni Serikali ya Marekani imeomba kutuma maafisa 18, hasa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Ulinzi, kwenda China ili kutoa msaada wa kiusalama na matibabu kwa wanamichezo wa Marekani wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing, na kwamba inaweza kuwasilisha maombi ya viza kwa maafisa wengine 40 baadaye.

Zhao amesema kuwa, Marekani inayoendeshwa na hila za kisiasa hapo awali ilielekeza na kuweka msimamo wa kutotuma ujumbe wa kidiplomasia au rasmi kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing ingawa hakuna mwaliko uliotolewa kwao.

Msemaji huyo amesema, China itashughulikia ombi la Marekani la kutuma timu ya maafisa wa serikali nchini China na maombi yao ya viza kwa mujibu wa desturi ya kimataifa, kanuni husika na kanuni ya usawa.

"Kwa mara nyingine tena tunaitaka Marekani kufuata moyo wa Olimpiki kwa vitendo, kujiepusha na kuingiza mambo ya siasa kwenye michezo, na kuacha maneno na vitendo potovu vinavyovuruga au kudhoofisha Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing," Zhao amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha