China yapunguza orodha hasi kwa uwekezaji wa kigeni kwa miaka 5 mfululizo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 28, 2021

Wafanyakazi wakipima malighafi kwenye karakana ya yabisi ya Kampuni ya Bayer HealthCare, Tawi la Qidong huko Qidong, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Desemba 2, 2020. (Xinhua/Zhang Yuwei)

BEIJING – Jumatatu ya wiki hii China imezindua orodha mbili zilizopunguza maeneo hasi kwa uwekezaji wa kigeni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufungua zaidi uchumi na kukuza maendeleo ya uchumi wenye kiwango cha juu.

Huu ni mwaka wa tano mfululizo ambapo nchi hiyo yenye nafasi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani imerekebisha orodha yake hasi ya kitaifa na orodha hasi ya eneo la jaribio la biashara huria (FTZ).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa pamoja na Kamati ya Kitaifa ya Maendeleo na Mageuzi (NDRC) na Wizara ya Biashara ya China, idadi ya maeneo ambayo hayaruhusiwi kuwekezwa kwa wawekezaji wa kigeni itapunguzwa hadi kufikia 31 katika toleo la Mwaka 2021 la orodha hasi ya kitaifa kutoka 33 katika toleo la Mwaka 2020.

Idadi ya maeneo kwenye orodha hasi ya eneo la jaribio la biashara huria (FTZ) itapunguzwa hadi 27 kutoka 30 katika toleo la Mwaka 2020.

Orodha hizo mbili mpya za sekta hasi zitaanza kutekelezwa Januari 1, 2022.

Kwa mujibu wa orodha mpya, vikomo vya umiliki wa hisa wa kigeni kwa kampuni za kutengeneza magari ya abiria vitaondolewa. Sekta zote za utengenezaji bidhaa zitafunguliwa kwa wawekezaji wa kigeni katika eneo la jaribio la bishara huria FTZ.

Nafasi ya wawekezaji wa kigeni katika kuwekeza kwenye sekta ya huduma katika eneo la jaribio la FTZ pia itapanuliwa. Uwekezaji wa kigeni utaruhusiwa katika sekta ya uchunguzi wa kijamii, lakini umiliki wa wawekezaji wa kigeni haupaswi kuzidi asilimia 33 na wawakilishi wa kisheria wanapaswa kuwa na uraia wa China.

Afisa kutoka NDRC amesema kwamba, kwa sekta ambazo hazijajumuishwa katika orodha hasi, kampuni kutoka nje ya China zinapaswa kupewa huduma sawa na kampuni za ndani.

China imeendelea kuwa thabiti katika kufungua uchumi kwa upana na kurahisisha zaidi mitaji ya nchi za nje kuingia nchini humo, na pia kuboresha mazingira yake ya biashara katika miaka iliyopita,. Idadi ya sekta zilizopigwa marufuku kwa wawekezaji wa kigeni imepunguzwa sana.

Wakati huo huo, hatua kadhaa kubwa za kufungua mlango wa kiuchumi zimetekelezwa katika sekta mbalimbali zikiwemo mambo ya fedha na utengenezaji wa magari, na hivyo kutoa nafasi kubwa zaidi kwa uwekezaji wa kigeni.

Kutokana na kushuka kwa kasi ya uwekezaji wa kimataifa wa kuvuka mpaka kote duniani, China ilivutia uwekezaji wa kigeni wa dola za Marekani bilioni 149.34 kwa Mwaka 2020, na kudumisha nafasi ya pili ya kupokea uwekezaji mwingi zaidi wa kigeni duniani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha