Biashara kati ya China na wanachama wengine wa RCEP yakaribia yuan trilioni 11

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 30, 2021

BEIJING – Uagizaji na uuzaji bidhaa nchi za nje kati ya China na nchi wanachama wengine 14 wa Ushirikiano Kamili wa Kiuchumi wa Kikanda (RCEP) umefikia yuan trilioni 10.96 (sawa na dola za Kimarekani trilioni 1.72) katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka huu wa 2021.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumatano wiki hii kutoka Mamlaka ya Forodha ya China (GAC), takwimu hiyo inachangia asilimia 31 ya thamani ya jumla ya biashara ya nje ya China.

Taarifa imesema, China imechukua hatua za kuimarisha zaidi biashara kati yake na nchi wanachama wengine wa RCEP, ikiwa ni pamoja na kuzifahamisha kampuni taratibu zinazofaa za kuagiza bidhaa na kuuza nje na kuendeleza utambuzi wa pande zote wa Waendeshaji Uchumi Walioidhinishwa (AEOs) na wanachama watano wa RCEP.

Mfumo wa AEO, ulioanzishwa na Shirika la Forodha Duniani, unalenga kuwezesha upatikanaji wa kibali cha forodha kwa kampuni za biashara kupitia mashirika ya forodha kuthibitisha kampuni zenye viwango vya juu vya kufuata sheria na usalama, na kiwango kizuri cha uaminifu.

Taarifa hiyo imeeleza, China tayari imetia saini makubaliano ya pande zote ya AEO na wanachama watano kati ya 10 wa RCEP ambao wamepitisha mfumo wa AEO, na inatafuta makubaliano hayo na wanachama wengine watano.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Ushirikiano Kamili wa Kiuchumi wa Kikanda (RCEP), hadi sasa nchi 10 za ASEAN ambazo ni Indonesia, Thailand, Singapore, Malaysia, Ufilipino, Vietnam, Brunei, Cambodia, Myanmar na Laos zimetia saini ushirikiano huo wa kichumi. Na nchi za Australia, New Zealand, China, Japan na Korea Kusini nazo pia zimeingia kwenye ushirikiano huo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha