Serikali ya Hong Kong kuwa thabiti katika kulinda Usalama wa Taifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 31, 2021

HONG KONG - Serikali ya Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong (HKSAR) wa China imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba itakuwa thabiti na itachukua juhudi zote katika kukabiliana na shughuli zozote zinayodhoofisha usalama wa taifa.

Katika taarifa yake ya Alhamisi wiki hii, Idara ya Usalama wa Taifa ya Jeshi la Polisi la Hong Kong imesema, Jumatano asubuhi iliwakamata wafanyakazi sita wa sasa au wa zamani wa Chombo cha Habari cha Mtandaoni cha Stand News huko Hong Kong, kwa tuhuma za njama ya kuchapisha uchapishaji wenye uchochezi, kinyume na kifungu cha 9 na 10 cha Sheria ya Uhalifu.

Msemaji wa Serikali ya HKSAR ametoa taarifa akisema kwamba hatua za utekelezaji wa sheria zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi la Hong Kong dhidi ya Stand News ni madhubuti kwa mujibu wa sheria na kwa msingi wa ushahidi, na kwamba Serikali ya HKSAR imedhamiria kukabiliana na vitendo na shughuli zinazohatarisha Usalama wa Taifa kwa mujibu wa sheria.

Msemaji huyo amebainisha kuwa, uhuru wa kutoa maoni na wa vyombo vya habari unalindwa chini ya Sheria ya Msingi na Sheria ya Haki za Binadamu ya Hong Kong. Kifungu cha 4 cha Sheria ya Usalama wa Taifa ya Hong Kong pia kinabainisha kuwa haki na uhuru huo utalindwa kwa mujibu wa sheria ili kulinda usalama wa taifa ndani ya HKSAR.

Msemaji huyo amesema, kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa, uhuru wa kutoa maoni na wa vyombo vya habari una mipaka na unaweza kuwekewa vikwazo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kulinda usalama wa taifa. Amesisitiza kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Msemaji huyo pia ameelezea masikitiko makubwa ya Serikali ya HKSAR kuhusu jaribio la Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi kupotosha ukweli wa mambo na kutoa kashfa juu ya hatua za utekelezaji wa sheria kwa mujibu wa sheria.

"Hatua zilizochukuliwa na Polisi katika tukio hii zililenga vitendo haramu vya waliokamatwa, na havihusiani na uhuru wa vyombo vya habari na uchapishaji," msemaji huyo amesema na kuongeza kuwa vitendo kama hivyo vya nchi za Magharibi vinaingilia kati kwa kiasi kikubwa mambo ya Hong Kong, na vinaakisi vigezo vyao viwili.

Msemaji huyo amesema kuwa Serikali ya HKSAR itaendelea kujilinda dhidi ya vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama wa taifa, na mtu au taasisi yoyote inayokiuka sheria itafikishwa mahakamani bila kujali hadhi yake.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha