Salamu za mwaka mpya za Rais Xi Jinping wa China

(CRI Online) Januari 04, 2022

(Picha inatoka CRI.)

Hamjambo! Mwaka 2022 unawadia, nikiwa hapa Beijing, nawapa nyote salamu za mwaka mpya.

Mwaka uliopita ulikuwa mwaka wenye maana ya kipekee. Tumeshuhudia mambo makubwa katika historia ya Chama chetu cha Kikomunisti cha China na taifa letu. Malengo mawili ya miaka mia moja yamekutana kihistoria, tumefunga safari mpya ya kujenga nchi ya kisasa ya kijamaa kwa pande zote, na tukiwa na nia imara tunasonga mbele kwenye njia ya kutimiza ustawi mpya wa Taifa la China.

Kuanzia mwanzoni hadi mwishoni mwa mwaka huo, watu wanaofanya kazi mbalimbali za kilimo, viwanda, jumuiya za makazi ya umma, shule, hospitali, majeshi, utafiti wa kisayansi na nyinginezo wamefanya bidii kwa mwaka mzima, na wamepata mafanikio. Wakati unapita kwa haraka, tumeona na kutambua kuwa, China ni nchi yenye ujasiri na ustawi. Katika nchi hii, kuna watu wema na waheshimiwa, kuna maendeleo yanayotokea kila siku, na kuna shughuli kubwa zinazorithishwa kizazi baada ya kizazi.

Julai Mosi, tulisherehekea kwa shangwe maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Niliposimama kwenye mnara wa Tian’anmen, niliguswa sana nilipokumbuka kuwa katika safari ya kihistoria iliyojaa mabadiliko na sintofahamu, wanachama wa CPC wameongoza mamia ya mamilioni ya wananchi kupita kwenye magumu na hatari kwa dhamira na ushupavu, na hatimaye kufanikisha mafanikio makubwa ya CPC kilichotimiza miaka mia moja. Tusisahau nia yetu ya asili, ndivyo lengo letu la msingi litakavyotimizwa. Tunatakiwa kufanya bidii bila kusita, ndivyo tutakavyofikia majukumu ya historia, matakwa ya zama, na matarajio ya watu.

Mkutano wa Sita wa Kamati Kuu ya 19 ya CPC ulipitisha azimio la tatu la kihistoria la Chama. Mafanikio yaliyopatikana katika miaka mia moja iliyopita yanasisimua, na uzoefu tulioupata katika miaka mia moja iliyopita umetupa busara. Niliwahi kuelezea maongezi ya zamani kati ya mwenyekiti Mao na Bwana Huang Yanpei, tunatakiwa kuthubutu kujitathmini ili kunyakua nafasi bora katika historia. Ustawi mpya wa Taifa la China kamwe hauwezi kufanikishwa kirahisi kwa kupiga kelele tu, na wala pia hautakuwa safari fupi na rahisi kwenye barabara tambarare. Tunapaswa kuangalia mbali, tuchukue tahadhari wakati tuko salama, kudumisha vipaumbele vya kimkakati na uvumilivu, ili kuweza “kutimiza malengo makubwa na mapana na vilevile kuzingatia masuala madogo madogo kadri inavyowezekana”.

Nchi kubwa huwa na mambo mengi mazito. Kimsingi yote yanawahusisha wananchi na familia mbalimbali. Nilifanya ziara katika sehemu mbalimbali, nikajionea hali halisi na kupata mawazo na msukumo mkubwa. Kila nilipowatembelea wananchi nyumbani, niliwauliza, mna kero gani? Waliyoniambia yote nayakumbuka moyoni. Kero zinazowasumbua wananchi, lazima nifuatilie, na matarajio yao, ni lazima niyatekeleze. Mimi natoka sehemu ya kijijini, najua vizuri taabu ya umaskini. Kutokana na juhudi za kizazi baada ya kizazi, wananchi waliouishi umaskini hivi sasa wana chakula, nguo, elimu, malazi na kulindwa na bima ya afya. Kuondokana na umaskini na kuleta maisha bora ni ahadi ya chama chetu kwa wananchi, pia ni mchango wetu kwa Dunia nzima. Hatuwezi kubweteka na mafanikio yaliyopatikana sasa, kwani bado kuna njia ndefu mbeleni tukielekea lengo la kufanikisha maisha mazuri zaidi ya kila mwananchi.

Utulivu wa Mto Manjano ni matarajio ya milenia ya watu wa China. Katika miaka michache iliyopita, nimetembelea mikoa yote tisa kwenye sehemu za juu, kati na chini za mto huo. Kutoka Mto Manjano na Mto Yangtze, ambayo ni "mito mama" miwili ya Taifa la China, hadi Ziwa Qinghai lenye maji angavu na Mto mkubwa wa Yarlung Zangbo; kutoka mradi wa kupeleka maji kutoka Kusini kwenda Kaskazini, unaojulikana kama mradi mkuu wa karne hii, hadi msitu wa Saihanba, ambao ulikuwa jangwa na sasa unaoneshwa kama sehemu ya kijani kibichi kwenye ramani; kutoka safari ya Kaskazini na kurudi nyumbani kwa tembo katika Mkoa wa Yunnan, hadi kuhama na kurudi kwa paa wa Tibet - yote haya yanatukumbusha kwamba "Tusipoharibu mazingira ya asili, kamwe mazingira ya asili hayatatuangusha ".

Mwaka huu pia umerekodi sauti nyingi za kukumbukwa za Wachina, matukio ya Wachina na hadithi za Kichina: viapo vya ujana vya "kuahidi kwa Chama kuifanya nchi yangu kuwa imara"; maelezo yenye mvuto ya "upendo halisi, na wa kweli unahifadhiwa kwa ajili ya taifa"; Chombo cha kuchunguza Sayari ya Mars cha Zhurong, satelaiti ya Xihe inayozunguka jua, na kituo cha anga ya juu cha Tianhe kinachosafiri miongoni mwa nyota; wanamichezo walioshindana kwenye viwanja vya michezo; taifa zima kuwa na umoja katika kukabiliana na COVID-19; watu katika maeneo yaliyokumbwa na maafa wakisimama pamoja ili kujenga upya makazi yao; askari wa Jeshi la Ukombozi la Watu na Polisi wenye Silaha waliojitolea kujenga jeshi lenye nguvu na kulinda nchi yetu. Kazi ngumu na kujitolea kwa mashujaa wengi ambao hawatajwi, vyote vimeongeza kasi kubwa ya kusonga mbele kwa China katika enzi mpya.

Ustawi na utulivu wa Hong Kong na Macao daima unafuatiliwa. Ni kwa umoja na juhudi za pamoja tu, ndipo tunaweza kuhakikisha utekelezaji mzuri wa sera ya “Nchi Moja, Mifumo Miwili” kwa muda mrefu. Kuunganishwa tena kamili kwa nchi yetu ni nia ya pamoja ya watu wa pande zote za Mlango-Bahari wa Taiwan. Ninatumai kwa dhati kwamba wana na mabinti wote wa Taifa la China, wataungana ili kujenga mustakabali mwema wa taifa letu.

Nilipoongea na viongozi wa nchi nyingine na wakuu wa mashirika ya kimataifa kwa njia ya simu au video, nimesikia mara nyingi pongezi kwa China kwenye mapambano dhidi ya janga la COVID-19 na mchango katika mwitikio wa kimataifa kwenye mapambano dhidi ya janga hilo. Hadi sasa, China imetoa dozi bilioni mbili za chanjo dhidi ya COVID-19 kwa zaidi ya nchi 120 na mashirika ya kimataifa. Ni kupitia umoja, mshikamano na ushirikiano pekee ndipo nchi zote duniani zinaweza kufungua ukurasa mpya katika kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Baada ya mwezi mmoja tu, Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya Baridi itafunguliwa hapa Beijing. Ushiriki mkubwa wa umma katika michezo ya majira ya baridi pia huchangia Harakati za Olimpiki. Hatutaacha juhudi zozote kuandaa vizuri Michezo hii kwa ajili ya Dunia. Dunia imeelekeza macho yake kwa China, na China iko tayari.

Kengele inakaribia kulia kukaribisha Mwaka Mpya. Hivi tunavyoongea, wanaanga watatu wa China wako kazini kwenye anga ya juu; wenzetu walioko nchi za nje bado wanafanya kazi kwa bidii sana; watu wetu waliotumwa kwenye balozi zetu na biashara nje ya nchi, na wanafunzi Wachina walioko ng'ambo wanavumilia kwa ujasiri; na watu wetu wanaotafuta ndoto zao wanaendelea na kazi zao vizuri. Nawapongeza kwa juhudi zenu kubwa, na ninawatakia kila la heri ya Mwaka Mpya.

Hebu sote tufanye kazi pamoja kwa ajili ya mustakabali wa pamoja. Naitakia nchi yetu mafanikio na watu wetu waishi kwa amani na masikilizano!

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha