Raia wa kigeni walioko Xi'an wajawa na matumaini huku Visa vya UVIKO-19 vikiibuka tena

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 05, 2022

XI'AN - Sandrine, raia wa Ufaransa anayeishi Xi'an, mji wa kale Kaskazini-Magharibi mwa China, aliamua kuupokea Mwaka mpya wa 2022 kwa njia tofauti kidogo, kufanya kazi ya kujitolea ya kudhibiti na kuzuia janga la virusi vya korona katika mji huo.

Mji wa Xi’an ulioko Mkoa wa Shaanxi kwa sasa uko kwenye mapambano dhidi ya wimbi jipya la Janga la UVIKO-19, na visa zaidi ya 1,700 vimeripotiwa tangu Desemba 9, 2021, wakati viongozi wamechukua hatua kali kuzuia kuenea kwa virusi hivyo vya korona.

Kila mtu katika mji huo mkubwa wenye watu wapatao milioni 13 wakiwemo wenyeji, wahamiaji na watu kutoka nje ya nchi wameungana ili kuzishinda nyakati za majaribu ya virusi hivyo.

Wakazi wakiwa kwenye foleni kupima virusi vya korona kwenye kituo cha kupima UVIKO-19 huko Xi'an, Mkoa wa Shaanxi Kaskazini-Magharibi mwa China, Desemba 21, 2021. (Xinhua/Li Yibo)

Mtaalam wa Afya kutoka Ufaransa katika siku ya mwisho ya Mwaka 2021

Sandrine amekuwa mkazi wa Xi'an kwa karibu muongo mmoja na anajulikana zaidi kwa jina lake la Kichina, "Wu Hong."

Kabla ya usiku kuingia, alifika katika kituo cha kupima virusi vya korona katika Chuo Kikuu cha Northwestern Polytechnical (NPU), akavaa mavazi ya kujikinga, barakoa na miwani, na kuanza kazi yake.

Tangu kuzuka tena kwa janga hili, vituo zaidi 5,000 vya kupima virusi vya korona vimeanzishwa katika mji wote wa Xi’an, na wataalam wa afya, wafanyakazi wa jamii na watu wa kujitolea zaidi ya 100,000 wanazunguka kwenye vituo hivyo kulinda mji huo.

"Tunapaswa kufanya kazi pamoja ili kudhibiti janga hili, na hakuna kitu muhimu zaidi kuliko hili kwa sasa," Sandrine, ambaye anafundisha kalkulasi na masomo mengine yanayohusiana na hesabu katika NPU anasema.

"Kama mmoja wa wanajamii wa shule, ninahisi kuwa na wajibu wa kujiunga na vita dhidi ya janga hili," anaongeza. "Nikiwa mwalimu, napaswa kusimama na kuwalinda wanafunzi wangu pia."

Sandrine, raia wa Ufaransa anayejulikana zaidi kwa jina lake la Kichina "Wu Hong," akifanya kazi ya kujitolea kwenye kituo cha kupima virusi vya korona katika Chuo Kikuu cha Northwestern Polytechnical huko Xi'an, Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini-Magharibi mwa China, Desemba 29, 2021. (Xinhua)

Kushikamana pamoja kama Jumuiya

Dev Raturi, ni Raia wa India mwenye umri wa miaka 45, amekuwa akiishi nchini China kwa miaka 17. Mwaka 2012, alifungua mgahawa wake wa kwanza huko Xi'an.

Tangu Desemba 23, 2021, mitaa ya makazi imefungwa, na Raturi anaona kuwa ni baraka kwa kuwa imemruhusu kutumia wakati mzuri nyumbani. "Huu ni wakati mzuri wa kujifunza, kufanya mazoezi na kufurahia na familia yangu."

Dev Raturi, Raia wa India mwenye umri wa miaka 45, akipika chakula nyumbani wakati akiwa karantini huko Xi'an, Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini-Magharibi mwa China, Desemba 27, 2021. (Xinhua)

Ingawa wamefungiwa ndani katika kipindi hiki, maisha yao hayajaathiriwa sana.

"Tunalazimika kupima virusi vya korona karibu kila siku ili tuweze kujua hali zetu za afya," Raturi anasema, akiongeza kuwa wafanyakazi wa jamii ndiyo wanaohusika na ugawaji wa chakula na huduma zingine muhimu.

Raturi anamiliki mikahawa mitano mjini Xi'an na yote imefungwa kwa muda. "Ni hasara kubwa, lakini hasara ya muda mfupi tu. Ikiwa hutadhibiti (janga), itakuwa hasara ya muda mrefu, na tutapaswa kufunga migahawa milele," anasema.

Mfamasia akitayarisha dawa za mitishamba za Kichina (TCM) katika hospitali ya Xi'an TCM huko Xi'an, Mkoa wa Shaanxi Kaskazini-Magharibi mwa Uchina, Januari 3, 2022. (Xinhua/Li Yibo)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha