Spika wa Bunge la Tanzania ajiuzulu kwa ukosoaji wa deni la Taifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 07, 2022

DAR ES SALAAM - Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya uspika kufuatia kusambaa kwa kipande cha video ambacho kinamuonesha akikosoa mwenendo wa serikali wa kukopa akisema haukuwa na afya kwa nchi hiyo.

Katika taarifa yake iliyotolewa na Bunge mjini Dodoma Jana Alhamisi jioni, Ndugai amesema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumtaarifu kuhusu kujiuzulu kwake ambapo nakala ya barua pia ilipelekwa kwa Katibu wa Bunge.

“Kujiuzulu kwangu ni jambo la kibinafsi na nina nia ya kulinda maslahi ya taifa langu, serikali na chama changu,” amesema Ndugai katika taarifa hiyo.

Kufuatia kusambaa kwa video hiyo na kuibua mjadala wenye hisia tofauti miongoni mwa wananchi, Jumatatu ya wiki hii Ndugai aliomba radhi hadharani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kauli alizozitoa mapema wiki iliyopita kuwa Tanzania iko hatarini kupigwa mnada kutokana na kuongezeka kwa deni la taifa.

"Kama nimesema neno lolote la kumkatisha tamaa rais katika harakati zake za kujenga nchi, naomba radhi kwake na kwa Watanzania wote kwa ujumla," Ndugai aliuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma, Makao Makuu ya Bunge na Serikali.

Hata hivyo, siku iliyofuata ya Jumanne wiki hii, Rais Hassan akiwa Ikulu ya Dar es Salaam, wakati akipokea ripoti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogharamiwa kwa mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa, alipuuza wakosoaji wa ukopaji wa serikali, akithibitisha nia ya utawala wake kutafuta mikopo zaidi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.

Alisema wasiwasi juu ya deni la taifa linalozidi kuongezeka hauna msingi.

Ndugai alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania Novemba 17, 2015. Kabla ya kuchaguliwa kwake, alikuwa Naibu Spika kuanzia Mwaka 2010 hadi 2015.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha