Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito wa utulivu nchini Kazakhstan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 07, 2022

Wanajeshi wakifanya doria nje ya Ikulu ya Rais huko Nur-Sultan, Kazakhstan, Januari 6, 2022. (Picha na Kalizhan Ospanov/Xinhua)

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi wiki hii na Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia hali ya Kazakhstan kwa ukaribu na kumekuwa na mawasiliano kadhaa kati ya Umoja huo na Serikali ya Kazakhstan, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya simu ya siku ya Alhamisi asubuhi kati ya mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu barani Asia Natalia Gherman na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan, Akan Rakhmetullin.

"Wakati wa mawasiliano hayo, Natalia Gherman kwa niaba ya Katibu Mkuu alisisitiza maombi ya kujizuia, kujiepusha na vurugu na kuhimiza mazungumzo ili kushughulikia hali hiyo," Dujarric amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini New York, Makao Makuu ya UN.

Kuhusu ripoti za waathirika, amesema ni vigumu kwa Umoja wa Mataifa kuzithibitisha.

"Lakini kilicho wazi ni kwamba maandamano yote yanapaswa kuwa ya amani. Watu wana haki ya kueleza malalamiko yao. Inatakiwa kufanywa kwa amani. Na vyombo vya usalama vinatakiwa kulinda haki hiyo na kuonesha kuchukua hatua za kujizuia kutumia nguvu," amesema.

Kuhusu taarifa za kuwasili kwa wanajeshi kutoka Shirika la Mkataba wa Usalama wa Pamoja (CSTO) huko Kazakhstan, Dujarric amesema Umoja wa Mataifa uliarifiwa Alhamisi asubuhi na CSTO juu ya kupelekwa kwa wanajeshi hao.

"Nadhani kwetu sisi, jambo la muhimu ni kwamba vikosi vya usalama, iwe ni vya Kazakh au kutoka nje ya Kazakh, vinapaswa kuzingatia viwango sawa vya haki za binadamu, ambavyo ni kuonesha kujizuia kutumia nguvu na kulinda haki za watu kuandamana kwa amani, " amesema msemaji huyo.

Dujaric amesema, jumla ya wafanyakazi 101 wa kimataifa na wafanyakazi wenyeji 530 wako chini ya mipango ya usalama ya Umoja wa Mataifa nchini Kazakhstan. Kila mtu yuko salama na wote wako katika uangalizi.

Kwa siku kadhaa sasa, wananchi nchini Kazakhstani wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ikiwemo miji ya Almaty na Mangystau. Maandamano hayo yaliyoanza kutokana na hasira juu ya serikali kuongeza kikomo cha bei ya gesi ya petroli ambayo Wakazakh wengi hutumia kuendesha magari yao, yamesababisha vifo kadhaa, majeruhi na uharibifu wa mali. Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan alitangaza hali ya dharuara huko Almaty na eneo la Magharibi la Mangystau kuanzia Januari 5 hadi Januari 19, 2022. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha