China yatoa Dozi milioni 10 zaidi za Chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 07, 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi akipokelewa na Raychelle Omamo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, mjini Mombasa, Kenya siku ya Alhamisi. TONY KARUMBA/AFP

MOMBASA, Kenya – Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema kwamba, China itatoa dozi milioni 10 zaidi za chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa Kenya kusaidia nchi hiyo kupambana na janga hilo.

Aidha, nchi hizo mbili za Kenya na China zimetia saini mikataba sita ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kutekeleza mipango ya ushirikiano ambayo China ilitangaza wakati wa Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika nchini Senegal mwezi Novemba mwaka jana.

Akizungumza wakati wa ziara yake barani Afrika siku ya Alhamisi katika mji wa pwani wa Mombasa, Wang amesema, Kenya ni mshirika wa kimkakati wa China siyo tu katika Afrika Mashariki, bali pia Afrika kwa ujumla kwani ni nguzo muhimu katika kutekeleza Pendekezo la Ukanda Mmmoja na Njia Moja barani humo.

"Katika mazungumzo yetu, tulishughulikia maeneo manne muhimu ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili. Haya ni: kuunga mkono uhuru, ushirikiano katika kufikia maendeleo ya kisasa na viwanda, na mshikamano katika kupunguza umaskini kadri tunapojitahidi kuwa na mustakabali wa pamoja na uwenzi katika amani ya kikanda na kimataifa," Wang amesema.

Pia amesisitiza umuhimu wa uhusiano kati ya China na Afrika kwa kueleza kuwa ziara yake ni sehemu ya desturi ya miaka 32 wa mawaziri wa mambo ya nje wa China katika kuifanya Afrika kuwa kituo cha kwanza cha ziara zao nje ya nchi kila mwaka.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Raychelle Omamo amesema, mikataba sita iliyotiwa saini na nchi hizo mbili ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya ambapo China imeahidi kuisaidia Kenya kuimarisha uwezo wake wa kutengeneza chanjo dhidi ya UVIKO-19 ndani ya nchi, pamoja na kutoa vifaa vya kuhifadhia chanjo baridi. Ameongeza kuwa China pia itatoa msaada wa tani 12,000 za mchele kwa familia zilizoathiriwa na janga hilo.

“Pia tumetia saini mikataba ya kushirikiana katika biashara, kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni wa China nchini Kenya, kupanua ushirikiano wetu wa kidijitali na kuungana mkono katika kukuza amani na usalama barani Afrika na kimataifa,” Omamo amesema.

Kuhusu lengo lake pana kwa Afrika, Wang amesema analenga kuhakikisha Afrika na China zinafikia malengo makuu matatu mwaka huu kadri pande hizo mbili zinaposhirikiana kukidhi matarajio ya FOCAC.

Uratibu wa uhusiano wa pande nyingi

"Kwanza, tunapanga kusimama pamoja kupambana dhidi ya janga la UVIKO-19, hasa kwa virusi vipya vya korona kama vile Omicron. Pia tunakusudia kushikilia masilahi ya pamoja katika siasa na kufanya uratibu wa kimataifa juu ya uhusiano wa kimataifa kwenye Umoja wa Mataifa katika kupigania haki za nchi zinazoendelea," Wang amesema.

"Makubaliano sita yaliyotiwa saini leo kati ya Kenya na China yanalenga mahsusi kuelekea lengo hilo," ameongeza Wang na kusisitiza kwamba China ina nia ya kuisaidia Afrika kutoka kwa umaskini.

Kenya ni nchi ya pili kati ya tatu ambazo Wang Yi amepanga kutembelea barani Afrika. Tayari amekwishatembelea Eritrea na baada ya Kenya ataelekea nchi ya Comoro. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha