Waasi wa Cameroon wanaotaka kujitenga walipua bomu katika mji mwenyeji wa AFCON

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 07, 2022

YAOUNDE – Taarifa za Jeshi la Polisi nchini Cameroon zinasema kwamba, wapiganaji wanaotaka kujitenga katika eneo lenye ukosefu wa amani linalozungumza Lugha ya Kiingereza, Kusini-Magharibi mwa Cameroon wamelipua vilipuzi (IED) katika Mji wa Limbe ambao utakuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Taarifa hiyo ya Polisi ya Alhamisi wiki hii imeeleza kwamba, hakuna aliyejeruhiwa katika mlipuko huo uliotokea mapema Alhamisi katika Mtaa wa Nusu Maili mjini humo ambao utakuwa mwenyeji wa mechi za Kundi F katika mashindano ya AFCON, kundi linalojumuisha nchi za Tunisia, Mali, Mauritania na Gambia.

Wapiganaji wanaotaka kujitenga na nchi ya Cameroon ambao wameapa kuvuruga mashindano ya AFCON katika mji huo wamesema kupitia mitandao ya kijamii kuwa wanahusika na mlipuko huo na kusisitiza kuwa ni "ishara ya onyo ya kile tutakachofanya wakati wa AFCON".

Viongozi wa kundi hilo walisema hawataki mechi za AFCON zifanyike katika eneo "linalokuwa na vita".

Jeshi la Cameroon limetuma silaha na wanajeshi zaidi katika eneo hilo ambao wanafanya doria za kawaida mchana na usiku.

Makundi ya wanaotaka kujitenga na Cameroon tangu mwaka 2017 yamekuwa yakipambana na vikosi vya serikali katika maeneo ya wazungumzaji wa Lugha ya Kiingereza (Anglophone) ya Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi ya nchi hiyo ambapo wanataka kuunda taifa huru wanaloliita "Ambazonia".

Mashindano ya AFCON yataanza rasmi Jumapili ya wiki hii katika Mji mkuu Yaounde na yatadumu kwa wiki nne.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha