

Lugha Nyingine
China kuharakisha miradi muhimu katika mpango wa 14 wa maendeleo wa Miaka Mitano
BEIJING – Baraza la Serikali la China limeamua kwamba, nchi hiyo itaharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa iliyoainishwa katika Mpango wa 14 wa maendeleo ya Miaka Mitano (2021-2025) ya kijamii na kiuchumi kwa kupanua uwekezaji.
Mkutano Mkuu wa Baraza la Serikali la China ulioongozwa na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang siku ya Jumatatu wiki hii umesema kwamba, kwa vile sera zinazotekelezeka na mipango ya kina imeandaliwa, mamlaka husika zinapaswa kuharakisha miradi mikubwa kwa hatua thabiti na kwa utaratibu.
Mkutano huo umebainisha kwamba, kwa sasa uchumi wa China uko katika kipindi muhimu, nchi hiyo inapaswa kutoa kipaumbele cha juu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuendeleza mkakati wake wa kupanua mahitaji ya ndani, na kuchukua hatua zinazolengwa ili kuongeza matumizi na uwekezaji.
Umeainisha kwamba, katika kusukuma mbele miradi yote mikubwa katika kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano, China itahakikisha ipasavyo fedha, matumizi ya ardhi na usambazaji wa nishati katika sekta muhimu kama vile usalama wa chakula na nishati, viwanda vya kiwango cha juu na vya teknolojia ya juu, usafirishaji na mawasiliano, na nyumba za mijini zenye ruzuku ya serikali.
Mkutano huo umeweka msisitizo katika kurahisisha taratibu za kiutawala kwa miradi hiyo iliyo tayari kutekelezwa, hasa miradi mikubwa ya uhifadhi wa maji, ili kuharakisha utekelezaji.
Katika ngazi za serikali za mitaa, mkutano umeamua kwamba China itatumia yuan trilioni 1.2 (sawa na dola za kimarekani bilioni 188.5) za bondi maalum za serikali za mitaa zilizotolewa katika robo ya nne ya Mwaka 2021, na kuharakisha utoaji wa dhamana ya 2022 iliyotolewa.
Mkutano huo pia umesisitiza kuongeza kasi ya uagizaji wa dawa kwa wingi, hasa dawa za magonjwa sugu na magonjwa ya kawaida, na vifaa vya matibabu vya thamani kubwa kama vile vipandikizi vya meno ili kupunguza zaidi gharama za matibabu.
Kwa mujibu wa mkutano huo, tangu ilipofika mwisho wa mwaka 2021, uagizaji wa kiserikali ulikuwa umesaidia kuokoa yuan bilioni 260 katika gharama za bima ya matibabu na matumizi ya huduma za afya kwa wagonjwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma