Madaktari wa Marekani wafanya upasuaji wa kwanza duniani wa kupandikiza moyo wa nguruwe kwa binadamu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 12, 2022

WASHINGTON - Katika upasuaji wa kwanza wa aina yake, mgonjwa Mmarekani mwenye umri wa miaka 57 aliye na ugonjwa mahututi wa moyo amepokea kwa kupandikizwa moyo wa nguruwe uliobadilishwa vinasaba na bado anaendelea vizuri kiafya hadi kufikia Jumanne ya wiki hii.

Baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa moyo ulio katika kipindi cha mwisho, mgonjwa huyo, David Bennett mwenye umri wa miaka 57, alionekana kutostahili kupandikizwa moyo katika Kituo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Maryland (UMMC) na vituo vingine vya upandikizaji kote nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa ya madaktari iliyotolewa na Kituo hicho Jumanne wiki hii, upasuaji huo uliofanywa katika UMMC Ijumaa ya wiki iliyopita, ulikuwa chaguo pekee linalopatikana kwa sasa kwa mgonjwa huyu.

Taarifa ya UMMC imesema kwamba, Bennett, mkazi wa Maryland, anaendelea kufuatiliwa kwa uangalifu kwa siku na wiki zijazo ili kubaini ikiwa upandikizaji huo unatoa faida za kuokoa maisha.

"Ilikuwa ni kufa au kufanya upandikizaji huu. Nataka kuishi. Najua ni risasi gizani, lakini ni chaguo langu la mwisho," amesema Bennett siku moja kabla ya upasuaji kufanywa. Alikuwa amelazwa hospitalini na hawezi kunyanyuka kutoka kitandani kwa miezi michache iliyopita.

Kwa mujibu wa UMMC, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani ilitoa idhini ya dharura ya upasuaji huo siku ya mkesha wa Mwaka Mpya kupitia utoaji wake uliopanuliwa wa upatikanaji huduma (matumizi ya huruma).

"Huu ulikuwa upasuaji wa mafanikio na unatuleta hatua moja karibu na kutatua tatizo la upungufu wa viungo (vya binadamu vya kupandikiza). Hakuna idadi ya kutosha ya watu wanaochangia mioyo kufikia orodha ndefu ya wagonjwa walengwa," amesema Bartley Griffith, ambaye ndiye daktari aliyefanya upasuaji huo wa kupandikiza moyo wa nguruwe kwa binadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya Marekani, takriban Wamarekani 110,000 kwa sasa wanasubiri kupandikizwa kiungo cha mwili, na zaidi ya wagonjwa 6,000 hufa kila mwaka kabla ya kupata mchango wa viungo hivyo vya mwili. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha