China yatangaza hatua za kudumisha utulivu wa biashara ya nje

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 12, 2022

Picha iliyopigwa Tarehe 13 Julai 2021 ikionesha meli iliyopakiwa makontena ikiondoka kwenye kituo cha kontena huko Lianyungang, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China. (Wang Jianmin/Xinhua)

BEIJING, Jan. 11 (Xinhua) -- China imezindua waraka mpya wa miongozo ya kupunguza shinikizo kwa kampuni za biashara ya nje na kuweka mauzo ya bidhaa na uagizaji bidhaa nje ya nchi katika hali ya utulivu.

Kwa mujibu wa waraka huo wa kuimarisha zaidi biashara ya nje uliotolewa na Baraza la Serikali ya China Jumanne wiki hii, China itafungua zaidi uchumi wake na kufanya marekebisho ili kusaidia kampuni za biashara ya nje ndogo na za kati kuhakikisha oda zao na kuleta utulivu wa matarajio.

Waraka huo umeeleza kwa kina hatua 15 zikiwemo uungaji mkono wa kisera na kifedha kwa kampuni za biashara ya nje pamoja na motisha kwa aina mpya za biashara katika biashara ya nje.

Kwa mujibu wa waraka huo, kiwango cha ubadilishaji wa fedha ya RMB ya China kitawekwa katika hali ya utulivu, katika kiwango mwafaka na chenye uwiano, na nchi hiyo itasaidia kampuni za biashara ya nje kukabiliana na hatari zinazotokana na kubadilisha fedha za kigeni.

Waraka umeeleza zaidi kwamba, China pia itachukua hatua za kupunguza hatari za mnyororo wa ugavi kwa kampuni za biashara ya nje na kuzihimiza kusaini mikataba ya muda mrefu na kampuni za usafiri wa meli.

Waraka huo umesisitiza juhudi za uagizaji wa bidhaa kuu kutoka nje ili kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa bidhaa hizo ndani ya nchi.

Waraka huo unaeleza kwamba, China itaimarisha zaidi biashara huria na hatua za kuirahisisha, na kuchukua utekelezaji wa Ushirikiano Kamili wa Kiuchumi wa Kikanda uwe fursa ya kuleta utulivu zaidi wa biashara ya nje. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha