China yaongoza duniani Kwa Mauzo ya Magari yanayotumia Nishati Mpya kwa miaka 7 mfululizo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 13, 2022

Mgeni akiangalia gari linalotumia nishati mpya (NEV) wakati wa shughuli ya kutangaza NEVs katika maeneo ya vijijini iliyofanyika Kunming, Mkoa wa Yunnan, Kusini-Magharibi mwa China, Desemba 4, 2020. (Xinhua/Jiang Wenyao)

BEIJING – Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, China imeorodheshwa katika nafasi ya kwanza duniani kwa mauzo ya magari yanayotumia nishati mpya (NEVs) kwa mwaka wa saba mfululizo Mwaka 2021, licha ya hali isiyokuwa na uhakika ya kiuchumi na shinikizo la mnyororo wa ugavi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari (MIIT) ya China, mauzo ya magari yanayotumia nishati mpya nchini humo yalifikia magari milioni 3.52 mwaka jana wa 2021.

"Sekta ya NEV (magari yenye kutumia nishati mpya) ya China ilidumisha kasi nzuri ya ukuaji katika uzalishaji na mauzo mwaka jana," amesema Fu Bingfeng, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Uzalishaji wa Magari la China, huku akisisitiza umuhimu wa mauzo thabiti ya NEV katika kuitikia mahitaji ya soko la magari la China.

Takwimu zinaonesha kwamba, uuzaji nje wa China wa magari yanayotumia nishati mpya, ulirekodi ukuaji mzuri mwaka jana, kwa magari 310,000 kuuzwa nje ya China.

Kuongezeka kwa mauzo ya magari yanayotumia nishati mpya kumekuja baada ya kuboreshwa kwa miundombinu nchini humo. Mwishoni mwa Mwaka 2021, China imejenga vituo 75,000 vya kuchajia, vifaa vya kuchaji milioni 2.62, na vituo 1,298 vya kubadilisha betri.

Guo Shougang, Afisa kutoka Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China (MIIT) anasema, hata hivyo, sekta ya magari yanayotumia nishati mpya nchini China bado inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa washindani wa kimataifa na changamoto za kuleta utulivu wa minyororo yake ya uzalishaji na ugavi.

Guo amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuzindua sera zenye nafuu zaidi za maegesho na kuchaji magari yanayotumia nishati mpya, na kuboresha sera za ununuzi wa magari hayo, ili kutoa mazingira mazuri ya kukuza mauzo zaidi.

Ameongeza kuwa wizara hiyo itaongeza juhudi katika kujenga vifaa zaidi vya kuchaji betri mnamo Mwaka 2022.

Takwimu hizo za Jumatano wiki hii pia zinaonesha kuwa uzalishaji na mauzo ya magari ya China yalipanda kwa asilimia 3.4 na asilimia 3.8 Mwaka 2021 kutoka mwaka mmoja uliopita, na hivyo kumaliza mwenendo wa kushuka kwa mauzo kwa miaka mitatu mfululizo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha