Nchi 8 wanachama wa UN zapoteza haki ya kupiga kura kutokana na kutokulipa ada za uanachama

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 13, 2022

Mwanamke akitembea kulipita jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Septemba 14, 2020. (Xinhua/Wang Ying)

UMOJA WA MATAIFA - Iran na Venezuela ni miongoni mwa nchi nane wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) ambazo haki zao za kupiga kura katika chombo hicho cha Dunia zimefutwa kutokana na kutolipa ada za uanachama.

Kwa mujibu wa Paulina Kubiak Msemaji wa Mwenyekiti wa Baraza la UN Abdulla Shahid, katika barua yake kwa Baraza Kuu siku ya Jumanne wiki hii, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres amesema jumla ya nchi 11 ziko nyuma katika malipo yao ya ada.

Paulina amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumatano wiki hii kwamba, kwa mujibu wa Kifungu cha 19 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, nchi mwanachama yenye malimbikizo ya malipo ya ada zake kwa kiasi ambacho ni sawa au kinachozidi michango inayodaiwa kwa miaka miwili iliyopita inaweza kupoteza kura yake katika Baraza Kuu.

“Isipokuwa inaruhusiwa ikiwa nchi mwanachama inaweza kuonesha kuwa ‘sababu zilizo nje ya uwezo’ zilichangia kutoweza kulipa ada,” Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema katika barua yake kwamba ndivyo itakavyokuwa kwa nchi za Visiwa vya Comoro, Sao Tome na Principe, na Somalia mwaka wa 2022 ambazo zimetoa sababu za kushindwa kulipa ada zao na kukubalika.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya Katibu Mkuu wa UN, Iran, Sudan, Venezuela, Antigua na Barbuda, Kongo, Guinea, Papua New Guinea na Vanuatu ni nchi nane ambazo hazina tena haki ya kupiga kura kwenye Baraza la UN.

Ili kila moja ya nchi hizi kurejesha kura yake, Guterres ametaja kiwango cha chini ambacho ni lazima kilipwe. Kwa mfano, Iran inahitaji kulipa dola za kimarekani milioni 18.4 na Venezuela dola milioni 39.8. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha