Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) nchini China wafikia rekodi ya juu Mwaka 2021

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2022

Picha ikionesha eneo la Majaribio la Biashara Huria la China (Shanghai) katika Eneo Jipya la Pudong huko Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Fang Zhe)

BEIJING, - Katika mwaka ambapo janga la UVIKO-19 liliendelea kuharibu uchumi wa Dunia, wawekezaji wa kimataifa wameongeza imani zaidi katika kuwekeza nchini China ambapo uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) ndani ya nchi hiyo ulifikia kiwango cha juu zaidi katika historia.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Alhamisi wiki hii na Wizara ya Biashara ya China, uwekezaji wa moja kwa moja katika China Bara uliotumika kihalisi, uliongezeka kwa asilimia 14.9 na kufikia kiwango cha juu ya yuan trilioni 1.15 Mwaka 2021.

Kwa mahesabu ya dola za kimarekani, uwekezaji huo wa kigeni nchini China ulipanda kwa asilimia 20.2 kufikia dola bilioni 173.48 za kimarekani.

Msemaji wa Wizara ya Biashara, Shu Jueting amewaambia waandishi wa habari kwamba, sekta za teknolojia ya juu zilishuhudia FDI ikiongezeka kwa asilimia 17.1 kutoka mwaka uliopita.

Uwekezaji wa kigeni katika sekta ya utengenezaji wa bidhaa za teknolojia ya juu na huduma za teknolojia ya juu nchini China ulipanda kwa asilimia 10.7 na asilimia 19.2 mwaka jana.

Zhang Jianping, mtafiti katika taasisi ya utafiti ya China ya Biashara ya Kimataifa na Ushirikiano wa Kiuchumi chini ya wizara ya biashara amesema, ukuaji huo mkubwa wa uwekezaji wa kigeni umetokana na msingi wa kiuchumi wa muda mrefu na imara wa China, na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara kila mara kumedumisha mvuto kwa mtaji wa kigeni.

Mwaka jana, jumla ya uingiaji wa FDI katika sekta ya huduma uliongezeka kwa asilimia 16.7 kuliko mwaka jana wakati kama huo, hadi kufikia yuan bilioni 906.49.

Uwekezaji katika China Bara kutoka nchi zilizo kando ya Pendekezo la Ukanda Mmoja na Njia Moja na Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia uliongezeka kwa asilimia 29.4 na asilimia 29 takwimu kutoka wizara hiyo zinaonesha.

Shu amesema, China itapanua zaidi ufunguaji wake wa kiwango cha juu wa uchumi, kuboresha huduma zake kwa kampuni na miradi inayowekezwa na mitaji kutoka nje, na kufanya juhudi zaidi kuboresha mazingira ya biashara Mwaka 2022.

Mwishoni mwa Desemba, 2021, Serikali ya China ilizindua orodha mbili zilizopunguza maeneo hasi ya uwekezaji wa kigeni, ambazo zote zimeanza kutumika tangu Januari 1, 2022, kama sehemu ya juhudi za kufungua uchumi wake zaidi.

Maeneo ya kikomo kwa wawekezaji wa kigeni yamepunguzwa hadi 31 katika toleo la Mwaka 2021 la orodha hasi kutoka 33 katika toleo la Mwaka 2020, wakati orodha hasi ya 2021 ya uwekezaji wa kigeni katika maeneo ya majaribio ya biashara huria ilipunguza idadi ya maeneo ya kikomo kwa wawekezaji wa kigeni hadi 27 kutoka 30. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha