Watafiti wa Hong Kong watengeneza nyenzo mpya inayoweza kuua virusi vya korona

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2022

HONG KONG - Chuo Kikuu cha Ufundi cha Hong Kong (PolyU) kimetangaza Alhamisi ya wiki hii kwamba timu yake ya utafiti imefanikiwa kutengeneza "vifaa vya uchapishaji vya 3D vya kukabiliana na virusi" ambavyo vinaweza kuua virusi vya korona kwenye vifaa na maeneo mbalimbali vile vile virusi vya kawaida na bakteria.

Kwa mujibu wa watafiti wa PolyU, sehemu kuu ya nyenzo hiyo ni resini, iliyoongezwa na vimelea vya kuzuia virusi kama vile misombo ya cationic, kutoboa utando wa seli ya virusi na kuharibu muundo wake ili kuua virusi na bakteria.

Chris Lo, profesa msaidizi katika Taasisi ya Nguo na Mavazi ya PolyU, ambaye aliongoza timu ya utafiti huo, amesema kwamba majaribio ya maabara yalithibitisha nyenzo hiyo inaweza kuondoa zaidi ya asilimia 90 ya virusi ndani ya dakika 10 na kumaliza karibu virusi na bakteria wote kwenye vifaa na maeneo walipo kwa dakika 20.

Lo amesema kuwa nyenzo hiyo ilikuwa nyenzo ya resini yenye ufanisi wa juu wa kupambana na virusi. Kwa kutumia teknolojia ya uchapishaji ya 3D, inaweza kuzalishwa kwa njia tofauti kukidhi mahitaji tofauti.

"Kwa hivyo ni rahisi kubadilika na inaweza kutumika sana katika vituo vya umma kutoa msaada wa kuzuia janga la UVIKO-19 kwa jamii," Lo amesema, huku akiongeza kuwa gharama ya nyenzo hiyo ilikuwa chini.

Katika mwaka uliopita, timu ya utafiti imeshirikiana na mashirika tofauti kuzalisha vishikio vya mapipa ya kuchakata taka, vifuniko vya vitasa vya milango ya choo, vitufe kwenye lifti, mbao za breli na mengineyo, ikilenga kufanya majaribio zaidi ya ufanisi na uimara wa nyenzo hiyo katika kuua virusi.

Kan Chi-wai, mshiriki wa timu ya watafiti na profesa katika Taasisi ya Nguo na Mavazi ya PolyU amesema kuwa hata baada ya kutumika kwa mwaka mmoja, siyo tu kishikio cha pipa la kuchakata taka bado kiko katika hali nzuri, bali hakuna virusi vya korona.

Kan ameongeza kwamba, hii inathibitisha kwamba kiwango cha ufanisi wa vifaa hivyo hupungua hatua kwa hatua baada ya miaka mitatu ya matumizi, na inafaa katika kupambana na virusi na bakteria.

Lo amesema, timu hiyo tayari imetuma maombi ya hataza ya teknolojia na matumizi yake, na itaitumia nyenzo hiyo ya kuua virusi kwa madhumuni ya kibiashara katika siku zijazo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha