AfCFTA na washirika wenzi wazindua mfumo wa malipo wa kuvuka mipaka ili kukuza biashara barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2022

ACCRA - Sekretarieti ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA), Benki ya Afrika (Afrexim) na washirika wengine wamezindua Mfumo wa Malipo na Mapatano wa Afrika (PAPSS) siku ya Alhamisi ya wiki hii katika jitihada za kukuza biashara ya ndani ya Afrika.

Hatua hiyo imefuatia ufanisi wa majaribio ya mfumo huo katika nchi sita za Ukanda wa Fedha wa Afrika Magharibi zikiwemo Ghana, Nigeria, Gambia, Liberia, Guinea na Sierra Leone.

Akizindua mfumo huo, Makamu wa Rais wa Ghana Mahamudu Bawumia amesema PAPSS itakomesha utegemezi wa Afrika kwa sarafu za upande wa tatu katika kulipia miamala ndani ya bara hilo na kusaidia kuendesha biashara ya ndani ya nchi za Afrika ili kuchochea ukuaji wa viwanda na kukuza ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi barani Afrika.

"Hili ni suluhu kutoka ndani ya Afrika kwa tatizo la Afrika. Ni mafanikio ya kiutendaji na muhimu zaidi katika uunganishaji wa mfumo wa malipo katika bara hili tangu kupata uhuru kutoka kwa wakoloni. Hii ni hatua ya karibu zaidi ambayo tumefikia kama bara kuelekea maono ya kutoa sarafu ya pamoja,” ameongeza.

Makamu huyo wa Rais amepongeza dira ya sekretarieti ya AfCFTA na Benki ya Afrexim katika kuendeleza mfumo huo, akisema utanufaisha biashara ndogo na za kati, wazalishaji na wauzaji bidhaa nje katika ukanda wa biashara wa bara zima la Afrika lenye watu bilioni 1.2.

Bawumia amezitaka Benki Kuu za nchi kote barani Afrika kutengeneza swichi zao za kitaifa ili kurahisisha upatikanaji wa mfumo wa malipo na kuhakikisha uhamishaji wa fedha bila vikwazo.

Kwa upande wake, Wamkele Mene, Katibu Mkuu wa AfCFTA, amesema, "kuzinduliwa kwa mfumo wa PAPSS wa kibiashara leo umekuja wakati muafaka na utakuza biashara ya ndani ya Afrika kwa kiasi kikubwa kwa kufanya malipo ya kuvuka mipaka kutotegemea sarafu ya tatu. Italisaidia Bara la Afrika kuokoa hadi dola za kimarekani bilioni tano kila mwaka."

"Pamoja na utekelezaji wa AfCFTA, tutaona ongezeko la miamala ya biashara barani Afrika. Maendeleo haya yataleta mahitaji makubwa ya huduma za malipo ya gharama nafuu, ambayo ni msingi wa uhusiano muhimu kati ya PAPSS na utekelezaji wa AfCFTA," ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha