Mahakama Kuu ya Marekani yatengua amri ya Serikali Kuu ya lazima ya chanjo kwa kampuni kubwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 14, 2022

WASHINGTON - Mahakama ya Juu ya nchini Marekani imezuia kutekelezwa kwa sheria ya Utawala wa Rais Joe Biden inayowataka wafanyakazi katika kampuni kubwa za Marekani kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 au kupimwa mara kwa mara, lakini imeruhusu amri hiyo ya lazima ya chanjo kwa wahudumu wa afya wanaopokea fedha kutoka Serikali Kuu kuendelea.

Mahakama Kuu ilitoa uamuzi ambao Majaji 6 walipiga kura ya Hapana na Watatu walipiga kura ya Ndiyo hivyo kuzuia amri ya lazima ya chanjo kwa waajiri wa sekta binafsi, huku wengi wa majaji hao wa kihafidhina wakiegemeza uamuzi wao kwenye hoja kwamba Ikulu ya Marekani imevuka mipaka ya mamlaka yake kwa kuweka sheria iliyotungwa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi. (OSHA) kwa kampuni zilizo na wafanyakazi 100 au zaidi, kwa kuwa Bunge la Wawakilishi la Marekani (Congress) halijaipa OSHA mamlaka ya kutunga sheria kama hiyo. Amri hiyo ya lazima ya chanjo itaathiri zaidi ya watu milioni 80.

"OSHA haijawahi kuweka amri kama hiyo hapo awali. Wala Bunge la Congress halijafanya hivyo. Kwa kweli, ingawa Bunge la Congress limetunga sheria muhimu kushughulikia janga la UVIKO-19, limekataa kutunga hatua yoyote sawa na ile ambayo OSHA imetangaza hapa," yanasema maoni ya majaji waliopiga kura ya Hapana (walio wengi).

Majaji watatu wa Mahakama Kuu walipinga uamuzi huo wa mahakama hiyo. "Tunapokuwa na busara, tunajua kutobadilisha maamuzi ya wataalam, wanaofanya kazi ndani ya mamlaka ya Bunge la Congress yaliyowekewa mipaka na chini ya udhibiti wa Rais, ili kushughulikia hali za dharura," wameandika katika maoni yao ya tofauti.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Rais Biden ametoa wito kwa majimbo na kampuni kuhimiza "mahitaji ya kupewa chanjo ili kulinda wafanyakazi wao, wateja na jamii."

"Mahakama imeamua kwamba utawala wangu hauwezi kutumia mamlaka iliyopewa na Bunge la Congress kuhitaji hatua hii, lakini hiyo haitazuia mimi kama rais kutumia sauti yangu kutetea waajiri kufanya jambo sahihi kulinda afya na uchumi wa Wamarekani.” amesema.

Biden alitangaza sheria hizo za ulazima wa chanjo mnamo Septemba Mwaka 2021 kama njia ya kukabiliana na kuibuka tena kwa janga la UVIKO-19, kabla ya hatua zake hizo kuanza kukumbwa na upinzani mkali kutokana na msululu wa kesi nyingi zilizofunguliwa katika majimbo yanayoongozwa na Chama cha Republican. Makundi mengine ya wafanyabiashara, wakati huo huo, yalisema kuwa amri ya lazima ya chanjo ingesababisha wafanyakazi kuacha kazi zao wakati ambao biashara nchini humo tayari zinakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha