Vijana wa Rwanda wageukia biashara ya mianzi chini ya ushauri wa wataalam kutoka China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 17, 2022

KIGALI - Idadi inayoongezeka ya vijana wa Rwanda wamegeukia biashara ya kutengeneza samani za mianzi na sanaa za mianzi baada ya mafunzo ya ustadi kutoka kwa wataalam kutoka China katika jitihada za kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Rwanda.

Kituo cha mafunzo cha usindikaji wa mianzi (kutengeneza samani na usukaji) kiko katika Kituo cha Biashara cha Kuandaa Mafundi cha Masaka, wilaya ya Kicukiro ya Kigali, Mji Mkuu wa Rwanda, ambapo vijana wameshuhudia utengenezaji wa bidhaa za mianzi.

Wataalamu wa Timu ya Msaada wa Mianzi ya China nchini Rwanda wamekuwa wakifanya miradi ya mafunzo ya kulima, kusindika na kutumia mianzi nchini Rwanda tangu Mwaka 2009.

“Wataalamu wa China walianzisha kilimo na usindikaji wa mianzi nchini kwetu, walitusaidia vifaa vya kusindika mianzi na kutufundisha jinsi ya kulima mianzi, kuvuna na kuichakata na kuwa bidhaa za mwisho kwa matumizi ya nyumbani kama samani, vikapu, vishikio vya taa, mapambo, vijiti vya kuchokonoa meno na miongoni mwa mengine," Irenee Gumyushime, mmoja wa wanafunzi katika kituo hicho, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano maalum.

Anasema usindikaji wa mianzi umemwezesha yeye na wenzake kupata ujuzi na utaalamu unaohitajika ili kujiajiri wenyewe jambo ambalo ni la msingi katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini humo.

“Wataalamu wa China walitufundisha ustadi wa usindikaji wa mianzi na sasa mimi ni mtaalamu wa kutengeneza samani, pia mimi ni mkufunzi katika kituo hiki, nawashukuru wataalamu wa China kwa jitihada zao za kufanya maisha yetu kuwa bora kupitia mafunzo haya,” anasema Gumyushime.

Anabainisha kuwa, hivi sasa wanakabiliwa na changamoto ya kupata vifaa vipya vya kusindika mianzi, kwa sababu vifaa vilivyopo ni vya zamani na vimechakaa, akisema kuwa Msaada wa China nchini Rwanda ambayo imekuwa ikiwasaidia imeisha.

Gumyushime anasema katika kituo hicho kuna wanafunzi 20 wanaojishughulisha na usindikaji wa mianzi na tisa kati ya hao ni wanawake.

Jean de Dieu Niyonkuru, mwanafunzi mwingine katika kituo hicho, ameliambia Xinhua kwamba yeye ni mtaalamu wa kutengeneza samani za mianzi baada ya kujifunza kutoka kwa wataalam wa China.

"Nilijiunga na kituo hiki Mwaka 2015 ambapo nilipatiwa mafunzo na wataalamu wa China katika usindikaji wa mianzi kwa muda wa miezi sita. Pia nilitumia miezi mingine mitatu kwa mafunzo ya utekelezaji huku nikipokea msaada wa ushauri kutoka kwa Wachina," anasema Niyonkuru. "Wachina pia walinipa fursa ya kwenda China kupata mafunzo zaidi ya usindikaji wa mianzi. Sasa ninafanya vizuri sana. Kuna biashara nzuri ya bidhaa za mianzi."

Niyonkuru anahusisha mafanikio yake yote katika utengenezaji wa samani za mianzi na mafunzo ya utaalamu mkubwa alioupata kutoka kwa wataalamu wa China.

"Samani zangu zote za nyumbani, sanaa za ufundi na bidhaa zimetengenezwa kwa mianzi kwa sababu napenda sana bidhaa za mianzi, maisha yangu yanategemea usindikaji wa mianzi, nawashukuru Wachina kwa kuniunga mkono na wenzangu ili kuboresha maisha yetu kwa usindikaji wa mianzi," anasema Niyonkuru.

Akizungumza na Xinhua, Mtaalamu wa China katika kituo hicho, Yu Qinhong, anasema ametoa mafunzo kwa wanafunzi wa Rwanda katika kituo hicho jinsi ya kutengeneza bidhaa bora zinazotokana na mianzi ili kuvutia wateja wengi zaidi.

"Rwanda inafaa kwa kuendeleza sekta ya mianzi. Wana malighafi ya mianzi na idadi kubwa ya vijana na Wanyarwanda wanapenda bidhaa za mianzi," anasema Yu.

Yu anaona kuwa hali ya hewa kavu ya Rwanda inafaa kwa samani za mianzi, ambayo huzuia ukungu kuathiri samani za mianzi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha