Ukuaji wa Pato la Taifa la China warejea kwa kasi katikati ya changamoto na matarajio

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 18, 2022

Wafanyakazi wakichomelea vyuma kwenye karakana ya kutengeneza magari katika Mji wa Qingzhou, Mkoa wa Shandong, Mashariki mwa China, Februari 28, 2021. (Picha na Wang Jilin/Xinhua)

Picha iliyopigwa Desemba 7, 2021 ikionesha magari kabla ya kupakiwa kwenye meli ya mizigo kwenye Bandari ya Yantai, Mkoa wa Shandong, Mashariki mwa China. (Picha na Tang Ke/Xinhua)

Picha iliyopigwa Novemba 26, 2021 ikionesha Daraja la Yachihe la Barabara Kuu ya Guiyang-Qianxi katika Mkoa wa Guizhou Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Ou Dongqu)

BEIJING - Uchumi wa China umeimarika zaidi Mwaka 2021 licha ya kuibuka mara kwa mara kwa mlipuko wa virusi vya korona na mazingira magumu ya kimataifa, ikiwa ni ishara ya uwezo wa nchi hiyo katika kuhakikisha utulivu wa uchumi kwa mwitikio wa haraka wa sera.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) imesema Jumatatu ya wiki hii kwamba, Pato la Taifa la China (GDP) limeongezeka kwa asilimia 8.1 na kufikia yuan trilioni 114.37 (kama dola trilioni 18 za Kimarekani) mwaka jana.

Takwimu hizo zimeonesha kwamba, kasi hiyo ya ukuaji wa uchumi ilikuwa juu ya lengo la serikali la "zaidi ya asilimia 6" na kuweka wastani wa ukuaji wa miaka miwili kuwa asilimia 5.1.

China inaendelea kuongoza Dunia katika kufufua uchumi na udhibiti wa janga la UVIKO-19 Mwaka 2021, NBS imesema, huku ikionya juu ya mashinikizo matatu ya kupungua kwa mahitaji, mishtuko ya usambazaji biadhaa muhimu, na kudhoofika kwa matarajio huku kukiwa na mazingira yasiyotabirika ya kimataifa.

Mkuu wa NBS Ning Jizhe amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba, matumizi ya mwisho yamechangia asilimia 65.4 katika ongezeko la Pato la Taifa, wakati mauzo ya nje ya bidhaa yamechangia asilimia 20.9.

Ning amesema kwamba "Ukuaji wa Uchumi wa China ulikuwa wa kasi zaidi miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani mwaka jana," na kuongeza kuwa, Pato la Taifa la nchi hiyo linakadiriwa kufikia zaidi ya asilimia 18 ya jumla ya pato la Dunia na kuchangia karibu asilimia 25 ya ukuaji wa Pato la Dunia.

Katika uchanganuzi, takwimu hizo zimeonesha kuwa mauzo ya rejareja yamekuwa na ahueni kubwa katika ukuaji ambapo yaliongezeka kwa asilimia 12.5 kuliko mwaka uliopita. Uwekezaji wa mali zisizohamishika nao umerekodi ukuaji thabiti wa asilimia 4.9, huku pato la viwandani lililoongezwa thamani likipanuka kwa asilimia 9.6 kutoka mwaka uliopita.

Soko la ajira nchini China nalo limeonekana kuwa tulivu kwa ujumla, huku kiwango cha ukosefu wa ajira mijini kikifikia asilimia 5.1, ikiwa ni cha chini ikilinganishwa na lengo la serikali la "karibu asilimia 5.5."

Ning amebainisha kuwa, wastani wa Pato la Taifa kwa kila mtu la China (GDP per capita) umefikia karibu dola za Kimarekani 12,500 Mwaka 2021, na kuzidi wastani wa kimataifa.

Hata hivyo, taarifa ya NBS imeeleza kwamba, Mwaka 2022, mazingira ya uchumi wa jumla yatakuwa duni kwani vichocheo vya kiuchumi katika nchi zinazoendelea vinaondolewa wakati nchi zinazoendelea bado zinakabiliwa na changamoto kubwa zinazohusiana na janga la virusi vya korona linaloendelea, ambalo litasababisha mahitaji duni ya uuzaji bidhaa nje, vikwazo vya usambazaji na matarajio ya kimataifa yasiyo na uhakika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha