Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania: Kususia Michezo ya Olimpiki wanaoathirika ni wanamichezo

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 19, 2022

Filbert Bayi (wa kulia)

(Picha inatoka Instagram ya kiofisi ya TOC.)

DAR ES SALAAM - Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema kwamba kususia Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing Mwaka huu wa 2022 ni kuwaathiri wanamichezo ambao wamekuwa wakijiandaa kwa miaka minne ili kushiriki mashindano hayo yenye hadhi ya juu duniani.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Tovuti ya Gazeti la Umma yaliyofanyika hivi karibuni kwa njia ya mtandaoni, Filbert Bayi amesema suala la kususia michezo si geni lakini limekuwa na athari kubwa kwa wanamichezo.

“Hili suala la kususia michezo mikubwa kama Olimpiki halikuanza leo…mwisho wa yote watakaoathirika ni wanamichezo ambao wamekuwa wakijiandaa kwa miaka minne” amesema Filbert Bayi ambaye pia amewahi kuwa mshindi  wa Tanzania wa medali ya fedha katika mbio za Mita 3000 kuruka magongo kwenye Mashindano ya Olimpiki ya Moscow Mwaka 1980, medali anayoiona kama heshima kwa nchi yake.

Akizungumzia maandalizi ya Michezo ya Olimpiki, Bayi amesema kwamba, alikuwa mmoja wa ujumbe wa Tanzania uliohudhuria Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto ya Beijing Mwaka 2008 na alichoshuhudia ni mambo mengi mapya kama ujenzi wa miundombinu ikiwa ni pamoja na Uwanja maarufu wa Olimpiki.

Ameongeza kusema kwamba, pamoja na Tanzania kutopata medali katika mashindano hayo, alivutiwa sana na michezo mbalimbali ambayo amesema ilikuwa ya aina yake na kwamba, anaamini katika michezo ya Olimpiki ya mwaka huu ya Majira ya Baridi itakayofanyika Beijing nchini China kutakuwa na uboreshaji wa mambo mbalimbali pamoja na Kijiji cha Wanamichezo ikiwa ni sehemu ya ufanikishaji wa michezo hiyo.

Amesema kwamba, ingawa Tanzania haishiriki Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi kutokana na majira ya nchi hiyo kuwa ya joto, watanzania wamekuwa wakifuatilia michezo hiyo kupitia televisheni na mitandaoni na hutamani kuwa sehemu ya michezo hiyo maana baadhi yao wamekuwa wakitamani kupanda Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote Afrika ukiwa na theluji kwenye kilele chake.

“Kuupenda mchezo ni aidha kwa kuucheza au kuuona kwenye televisheni au mitandaoni. Kutokana na hali halisi ya nchi yetu ya joto na Michezo ya wakati wa Baridi huchezwa kwenye barafu, ushabiki wa (mchezo fulani) unakuwepo pale wachezaji wanaposhiriki michezo ya kuteleza kwenye barafu, wengine wanatamani kwenda Mlima Kilimanjaro ambako kuna barafu” anasema Filbert Bayi.

Katika mahojiano hayo, Bayi amehitimisha kwa kuutakia kila la kheri Mji wa Beijing, wandaaji wa Mashindano ya Olimpiki ya Majira ya Baridi mwaka huu wa 2022, Serikali ya China na Kamati ya IOC. 

Filbert Bayi (kulia) akishiriki moja ya mashindano ya riadha enzi hizo akiwa mwanamichezo wa kushindana kwenye riadha.

(Picha kwa hisani ya Filbert Bayi)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha