Hotuba ya Xi kwenye Mkutano wa WEF yaleta muafaka wa kuhimiza ufufuaji wa Uchumi Duniani - Wataalam

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 19, 2022

BEIJING – Wataalam wa Uchumi kutoka nchi mbalimbali Duniani waliohojiwa na Shirika la Habari la China, Xinhua wamesema kwamba hotuba ya Rais wa China Xi Jinping katika mkutano wa mtandaoni wa mwaka 2022 wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF 2022) uliofanyika Jumatatu wiki hii imeonesha uwajibikaji wa China, na kufikia maoni ya pamoja kuhusu kukabiliana na UVIKO-19 na kuhimiza ufufuaji wa uchumi wa Dunia.

"Njia sahihi ya maendeleo ya binadamu ni maendeleo ya amani na ushirikiano wa kunufaishana. Nchi tofauti na zenye ustaarabu tofauti zinaweza kustawi kwa msingi wa kuheshimiana, kutafuta maelewano na matokeo ya kunufaishana kiuchumi kwa kuweka kando tofauti," Xi alisema katika hotuba yake hiyo.

“Hotuba hiyo ya Xi imeongeza imani katika kuimarika kwa uchumi wa Dunia kwa sasa”, anasema Volker Tschapke, Rais wa heshima wa Jumuiya ya Prussia ya Ujerumani, akisisitiza kwamba amani na maendeleo bado ni kauli mbiu ya Dunia katika siku za usoni.

Tschapke amesema, Pendekezo la China la Ukanda Mmoja na Njia Moja limekuwa mfano wa kuigwa kwa nchi na ustaarabu mbalimbali kustawi kwa pamoja kwa kuheshimiana na kupata ushirikiano wa kunufaishana kwa kutafuta maelewano pamoja na kuheshimu tofauti.

Joseph Matthews, Profesa Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha BELTEI huko Phnom Penh, Cambodia amesema hotuba ya Xi imeonesha juhudi za China katika kuhimiza ushirikiano wa pande nyingi, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto za kimataifa kwa kutimiza maslahi ya pamoja na kuishi pamoja kwa amani.

"Hotuba ya Rais Xi inaonesha dhamira isiyoyumba ya China ya kudumisha uhusiano wa pande nyingi wa kweli na biashara huria, ambayo ni ufunguo wa amani ya Dunia, ufufukaji wa uchumi na maendeleo ya pamoja katika zama za baada ya janga la UVIKO-19," amesema.

"Mawazo ya Vita Baridi, maamuzi ya upande mmoja, kujilinda kibiashara, umwamba, na sera za kutonufaishana zinaweza tu kudhuru nchi zingine," Matthews amesema. "Nchi mbalimbali zinapaswa kuishi pamoja kwa amani, kunufaishana, na kuendeleza ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu."

Alvaro Echeverria, Makamu wa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Asia Pasifiki nchini Chile, amesema hotuba ya Xi imeonesha moyo wa ushirikiano na kuongeza imani kwa Dunia kuondokana na janga la UVIKO-19 ikiwa imara.

Echeverria ameeleza kufurahishwa na kauli ya Xi juu ya kufikia ustawi wa pamoja na kuyafanya mafanikio ya maendeleo yawanufaishe watu kwa upana zaidi na kwa usawa, akisema maoni ya Xi ni shirikishi na yenye muono wa mbele.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha