China yazindua mpango wa kuboresha mitandao ya usafirishaji ifikapo 2025

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 19, 2022

Picha iliyopigwa Juni 28, 2021 ikionesha Daraja la Yunwu la Barabara Kuu ya Duyun-Anshun katika Mkoa wa Guizhou, Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Tao Liang)

BEIJING - China imezindua mpango kuhusu malengo makuu ya maendeleo ya mtandao wa usafirishaji katika kipindi cha Mpango wa 14 wa Maendeleo ya Miaka Mitano (2021-2025).

Kwa mujibu wa nyaraka ya mpango huo iliyotolewa na Baraza la Serikali la China, reli za mwendo kasi zitaenea hadi jumla ya urefu wa kilomita 50,000 Mwaka 2025, kutoka kilomita 38,000 za Mwaka 2020, na reli za treni zenye kasi ya kilomita 250 kwa saa zinatarajiwa kuunganisha asilimia 95 ya miji iliyo na idadi ya watu zaidi ya laki 5.

Nyaraka hiyo inaonesha kwamba, China itakuwa na kilomita 165,000 za reli mwaka 2025, kutoka kilomita 146,000 ya miaka mitano iliyopita; zaidi ya viwanja vya ndege 270 vya abiria, kutoka 241; kilomita 10,000 za njia za treni za ardhini katika miji, kutoka kilomita 6,600; kilomita 190,000 za Barabara Kuu, kutoka kilomita 161,000; na kilomita 18,500 za njia za maji, kutoka kilomita 16,100.

Mfumo wa usafiri pia utazingatia zaidi uhifadhi wa mazingira. Asilimia 72 ya mabasi mijini yatatumia nishati mpya, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 66.2, na kiwango cha utoaji wa hewa ya ukaa katika sekta ya usafirishaji kitapungua kwa asilimia 5.

Kwa mujibu wa mpango huo, lengo kuu ni kufikia maendeleo jumuishi ifikapo Mwaka 2025, na mafanikio yanayoonekana katika mabadiliko ya mfumo wa kisasa wa uendeshaji usafiri na unaotilia maanani uhifadhi wa mazingira.

Katika malengo ya ifikapo Mwaka 2035, mpango huo unalenga kujenga "duara 1-2-3" kwa safari za abiria na usafirishaji wa mizigo.

Hii ina maana kwamba muda wa kusafiri ndani ya miji, na makundi ya miji, na kati ya miji mikuu nchini China utapunguzwa hadi saa moja, saa mbili na saa tatu kwa mtiririko huo. Barua zinazotumwa na huduma za haraka zinatarajiwa kufikia kwa siku moja ndani ya China, siku mbili kwa nchi jirani, na siku tatu kwa miji mikubwa duniani.

Mpango huo unaonesha kwamba, Mwaka 2025, usalama wa usafirishaji wa chakula, nishati na madini utakuwa na hakikisho kubwa zaidi, na minyororo ya usambazaji wa vifaa ya kimataifa italindwa vema zaidi.

Mpango huo unaeleza kuwa kutafanyika maboresho ya China kuunganishwa na mawasiliano ya kimataifa. Umebainisha kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya usafiri baina ya China na nchi jirani, kusukuma mbele maendeleo ya kiwango cha juu ya usafiri wa treni za mizigo kati ya China na Ulaya, na kujenga "Njia ya Hariri ya Angani " (Air Silk Road) na kadhalika.

 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha