“Kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa China kunasababishwa na sababu nyingi”

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 21, 2022

(Picha kwa hisani ya IC)

Maafisa wa afya wa China wamesema Alhamisi wiki hii kwamba, kupungua kwa idadi ya watoto wachanga wanaozaliwa nchini China katika miaka ya hivi karibuni kumechangiwa na kupungua kwa idadi ya wanawake walio katika umri wa kuzaa, mabadiliko ya mitazamo miongoni mwa vijana kuhusu ndoa na uzazi, na kupanda kwa gharama za malezi ya watoto.

Wamesema hatua madhubuti zaidi zitachukuliwa ili kuhimiza uzazi na kuwapunguzia mzigo wa malezi wazazi ili kupunguza hali ya kushuka kwa idadi ya watoto wachanga.

Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya China, takriban watoto milioni 10.62 walizaliwa nchini China mwaka jana wa 2021, ikishuka kutoka milioni 12 Mwaka 2020 ikiwa ni idadi ndogo zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka jana, pia, kiwango cha kuzaliwa watoto kilishuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu Mwaka 1978.

Yang Jinrui, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya ufuatiliaji wa idadi ya watu na maendeleo ya familia ya Kamati ya Afya ya China, amesema kupungua kwa idadi ya wanawake walio katika umri wa kuzaa, hasa wale walio katika umri unaofaa zaidi wa kuzaa watoto, ni sababu kuu inayochangia kupungua kwa kiwango cha uzazi.

Yang amesema idadi ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20 hadi 34 imekuwa ikipungua kwa wastani wa milioni 3.4 kila mwaka kuanzia Mwaka 2016 hadi Mwaka 2020. Mwaka jana, idadi hiyo ilipungua kwa milioni 4.73 mwaka hadi mwaka.

Aidha, amesema, kuchelewea kufunga ndoa miongoni mwa vijana na ukosefu wa nia ya kupata watoto kumechochea hali hiyo.

“Watu waliozaliwa miaka ya 1990 na 2000 ambao ndiyo wengi wa wale wanaoweza kufunga ndoa na kupata watoto siku hizi, wamepata elimu kwa muda mrefu zaidi na kukabiliwa na shinikizo kubwa zaidi la ajira,” amesema na kuongeza kuwa jambo hilo limesababisha wengi wao kuchagua kuahirisha kufunga ndoa au hata kutofunga ndoa kabisa.

"Gharama kubwa za uzazi na elimu pia vimezua wasiwasi miongoni mwa vijana," Yang amesema.

Sera zinazounga mkono uzazi zahimizwa

Kama matokeo, "kama kiwango cha kupungua kwa watoto wachanga wanaozaliwa kila mwaka kinaweza kupungua au la itategemea mabadiliko katika kiwango cha uzazi", amesema.

"Ni muhimu kwa China kuharakisha utekelezaji wa sera zinazounga mkono ili kuimarisha uzazi."

"Mikoa mingi imeongeza muda wa likizo ya uzazi kwa siku 30 hadi 90 na imesisitiza kukuza maendeleo ya huduma za shule za chekechea zenye nafuu katika sheria zao mpya," anasema Yang na kuongeza kuwa baadhi ya serikali za mitaa zimeamua kutoa ruzuku ya uzazi au ya nyumba. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha