Uvumbuzi wa kifedha kuboresha Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 21, 2022

Mgeni akitazama maelezo kuhusu sarafu ya kidijitali ya China (e-CNY) kwenye maonesho huko Beijing. [Picha/DU JIANPO/People’s Daily]

Jumla ya fedha zilizotengwa na sekta ya benki ya Beijing kwa ajili ya ujenzi wa kumbi za Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Mwaka 2022 na vifaa vya usaidizi imezidi yuan bilioni 78 (sawa na dola za kimarekani bilioni 12.3), ambapo yuan bilioni 34.07 tayari zimewekezwa, anasema Li Mingxiao, Mkurugenzi wa Ofisi ya Beijing ya Kamati ya Usimamizi wa Benki na Bima ya China.

Li amesema katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi wiki hii kwamba, fedha zilizobaki katika uwekezaji wa michezo hiyo zilikuwa yuan bilioni 24.21, ambapo yuan bilioni 2.96 zilitumika kwa ujenzi wa kumbi za Olimpiki za msimu wa baridi, yuan bilioni 20.56 kwa vifaa vya kuwezesha michezo na yuan milioni 684 kwa miradi inayohusiana na sekta ya barafu na theluji.

Kamati hiyo imehimiza taasisi za benki kuhakikisha zinatoa mikopo kwa miradi inayohusiana na Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ili kukidhi mahitaji ya ufadhili wa miundombinu, kurahisisha taratibu za kuidhinisha mikopo, kufanya uvumbuzi katika huduma za kifedha na kuongeza ufanisi wa huduma za kifedha.

Li amesema, baada ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi, shirika la udhibiti litakuza zaidi huduma za kifedha kwa biashara ndogo ndogo katika sehemu ya juu na chini ya mnyororo wa sekta ya barafu na theluji, pamoja na kutoa msaada wa kifedha kwa ukarabati wa kumbi baada ya michezo hiyo na vile vile uzalishaji na matumizi yanayohusiana na michezo ya barafu na theluji.

Liu Jin Mkuu wa Bank ya China (BOC) amesema kwamba, benki hiyo inayomilikiwa na Serikali ya China na ambayo ni mkopeshaji mkubwa wa mikopo ya kibiashara na mshirika rasmi wa Michezo ya Olimpiki na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya baridi ya Beijing 2022, imetoa mikopo zaidi ya yuan bilioni 60 kwa miradi inayohusiana na barafu na theluji katika mikoa, manispaa na mikoa inayojiendesha zaidi ya 10.

Benki hiyo pia itatoa huduma za malipo ya RMB ya kidijitali wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi kupitia App, na pochi za mkononi kama vile kadi za e-CNY na mikanda ya kuvaa mkononi.

Ili kukidhi masharti magumu ya kuzuia na kudhibiti UVIKO-19 wakati wa Michezo, BOC imepitisha hatua mpya za kuzuia maambukizi ya virusi vya korona, kama vile kutumia vifaa mbalimbali vya kupokea pesa na kulipa katika maduka yake ya muda yaliyoundwa kuhudumia washiriki wa Michezo ya Olimpiki.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Renato Lu)

Picha