Shughuli za Olimpiki haziathiriwa na hali ya janga la UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 24, 2022

Mazoezi ya sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ya Beijing 2022 yamefanyika kwenye Uwanja wa Taifa uitwao "Kiota cha Ndege," Januari 22, 2022. Takriban washiriki 4,000 walihusika katika mazoezi ya kila tukio la sherehe ya ufunguzi, wakijiandaa kwa sherehe ya ufunguzi itakayofanyika Februari 4. [Picha/Xinhua]

Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing 2022 imesema, watu 39 wanaohusika na Michezo hiyo wamekutwa na UVIKO-19 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing walipowasili kuanzia Januari 4 hadi Jumamosi ya Januari 22, 2022 wakati visa vingine vya UVIKO-19 vipatavyo 33 vimethibitishwa katika eneo lililofungwa kitanzi la michezo hiyo.

“Walioambukizwa ni washikadau na si wanamichezo” Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki na ya walemavu ya majira ya baridi ya Beijing 2022 imesema katika taarifa yake jana Jumapili.

Wshikadau ni pamoja na wafanyakazi wa utangazaji, wanachama wa mashirikisho ya kimataifa, wafanyakazi wa washirika wa masoko na matangazo ya kibiashara, wanafamilia wa maafisa wa Olimpiki na Paralimpiki na wafanyakazi wa vyombo vya habari na timu za wafanyakazi wengine.

Kwa mujibu wa toleo la hivi punde la Kitabu cha mwongozo kuhusu udhibiti wa UVIKO-19 cha Michezo ya Olimpiki ya Beijing 2022, washikadau hao watakapothibitishwa kuwa na UVIKO-19, watapelekwa katika hospitali zilizoteuliwa kwa matibabu iwapo watakuwa na dalili. Ikiwa hawana dalili, watapaswa kukaa katika kituo cha karantini.

Taarifa hiyo imesisitiza kwamba wafanyakazi wote wanaohusika na Olimpiki wanaoingia China na wafanyakazi wa Michezo lazima wafuate utekelezaji wa usimamizi wa eneo lililofungwa kitanzi la michezo hiyo, ambao chini yake wanatengwa kabisa na watu wa nje.

Kuanzia Januari 4 hadi Jumamosi ya Januari 22, watu 2,586 wanaohusiana na Olimpiki, wanamichezo 171 na maafisa wa timu na wadau wengine 2,415 waliingia China kupitia uwanja wa ndege. Baada ya kupimwa UVIKO-19 kwenye uwanja wa ndege, watu 39 walithibitishwa kuambukizwa virusi vya korona.

Taarifa imesema, katika eneo lililofungwa kitanzi la michezo ya Olimpiki, vipimo 336,421 vya UVIKO-19 vimefanywa na visa 33 vilithibitishwa.

Wafanyakazi wa kijiji cha Michezo ya Olimpiki watathibitisha kwa kila ujumbe wa timu za taifa za Olimpiki kuhusu taarifa za usajili wa wanamichezo watakaoingia humo, na kisha kuwaambia mahali vyumba vyao vilipo.

"Lengo letu ni kuwafanya wanamichezo wajisikie salama na wastarehe kama 'nyumbani' kwao. Kipindi cha majaribio ya uendeshaji Kijiji cha Olimpiki kati ya Jumapili na Alhamisi kitasaidia timu ya oparesheni kutoa huduma bora kwa washiriki wa Olimpiki," amesema Shen Qianfan, mkuu wa timu ya operesheni ya kijiji hicho.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha