Burkina Faso yatangaza marufuku ya kutoka nje kwa nchi nzima

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 24, 2022

OUAGADOUGOU - Amri ya kutotoka nje nchini kote imewekwa Jana Jumapili nchini Burkina Faso kuanzia saa 2 mchana hadi saa 11 na nusu asubuhi kwa saa za huko.

Kwa mujibu amri hiyo iliyotiwa saini na Rais Roch Marc Christian Kabore, marufuku imekuja kufuatia tukio la milio ya risasi katika baadhi ya kambi za jeshi asubuhi ya siku hiyo.

Taarifa nyingine kutoka kwa Waziri wa Elimu wa nchi hiyo ilitangaza kufungwa kwa shule siku ya Jumatatu (leo) na Jumanne wiki hii.

Milio ya risasi ilisikika mapema Jumapili asubuhi kwenye kambi za jeshi katika Mji Mkuu wa Ouagadougou na miji mingine. Serikali ya Burkina Faso ilithibitisha kutokea kwa milio ya risasi lakini ikakanusha taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu jeshi kufanya mapinduzi ya utawala wa kiraia na kuchukua uongozi wa Serikali ya nchi hiyo.

Waziri wa Ulinzi Jenerali Barthelemy Simpore alitangaza kupitia kituo cha televisheni cha taifa kwamba hali imedhibitiwa, na kukanusha uvumi kuwa rais amezuiliwa na wanajeshi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya nchi hiyo, baadaye mchana, makao makuu ya chama tawala cha Burkina Faso huko Ouagadougou yalichomwa moto na waandamanaji. Mtandao wa intaneti ulizimwa kwa sehemu.

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imetoa wito wa utulivu na kusisitiza uungaji mkono wake kwa Rais Kabore.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha