Utata wa Kisiasa waendelea Burkina Faso huku AU na UN zikilaani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 25, 2022

ADDIS ABABA – Utata wa kisiasa bado unaendelea kuikumba nchi ya Burkina Faso kufuatia milio ya risasi kusikika mapema Asubuhi ya Jumapili ya wiki iliyopita huku taarifa kinzani zikitolewa na pande zinazohusika.

Jioni Jumatatu ya wiki hii Jeshi la Burkina Faso lilitoa taarifa kwamba, Rais Roch Kabore ameondolewa madarakani huku chama tawala nchini humo kikisema mapema katika taarifa yake kwamba Rais Roch Kabore amenusurika katika jaribio la mauaji.

Hata hivyo, taarifa ya chama tawala imeongeza kuwa kile kilichoanza kama uasi wa baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Burkina Faso siku ya Jumapili ya wiki iliyopita kinabadilika kwa kasi na kuwa mapinduzi.

Katika taarifa ya awali ya Jeshi la Burkina Faso, ilielezwa kwamba jeshi hilo limemwondoa madarakani Rais Roch Kabore, kusimamisha matumizi ya katiba, kuvunja serikali na bunge la taifa, na kufunga mipaka ya nchi hiyo.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat, amelaani jaribio la mapinduzi ya serikali ya kiraia nchini Burkina Faso.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Jumatatu ya wiki hii, Moussa Faki amesema anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali mbaya nchini Burkina Faso na analaani vikali jaribio la mapinduzi katika nchi hiyo.

"Yeye (Faki Mahamat) anatoa wito kwa Jeshi la Burkina Faso na vikosi vya usalama vya nchi hiyo kuzingatia kwa dhati wito wao kwa jamhuri, yaani kulinda usalama wa ndani na nje wa nchi," inasema taarifa ya AU.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatatu ya wiki hii ametoa wito kwa wahusika wote nchini Burkina Faso kujizuia na kuchagua mazungumzo baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa rais madarakani katika mapinduzi ya hivi punde zaidi.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa "analaani vikali jaribio lolote la kuchukua serikali kwa kutumia silaha" na "anatoa wito kwa viongozi wa mapinduzi kuweka silaha zao chini," kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa UN Stephane Dujarric.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha