GDP ya mji wa Dongguan "Kiwanda cha Dunia" nchini China yazidi Yuan Trilioni 1

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 25, 2022

GUANGZHOU - Takwimu mpya zinaonesha kuwa mji wa Dongguan, uliopewa jina la "kiwanda cha Dunia," katika Mkoa wa Guangdong Kusini mwa China, umerekodi Pato (GDP) la zaidi ya yuan trilioni 1 (sawa na dola za Marekani bilioni 157.7) katika Mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.2 mwaka hadi mwaka.

Hii inaashiria kuwa Dongguan unakuwa mji wa 24 wa China ambao pato lake la uchumi limepita Yuan trilioni 1 hadi sasa. Hatua hii inadhihirisha zaidi uimara wa uchumi wa China.

Ikiwa kitovu cha biashara ya nje ya China, biashara ya nje ya mji huo imeathiriwa sana na janga la UVIKO-19 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ukosefu wa oda za bidhaa hapo awali na ukosefu wa wafanyakazi baadaye pamoja na uhaba wa makontena vyote kwa pamoja viliathiri biashara ya nje ya mji huo.

Hata hivyo, Januari 2021, kasi ya ukuaji wa biashara ya nje ya Dongguan iliacha kushuka na kuanza kuimarika. Thamani ya jumla ya uagizaji na uuzaji bidhaa kwa nje wa mwaka 2021 ilifikia yuan trilioni 1.52, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.6 kuliko mwaka uliopita.

Mwaka 2021, thamani ya bidhaa za viwandani zilizoongezwa thamani zinazozalishwa na kampuni kubwa za Dongguan ilifikia takriban yuan bilioni 500.9, ambayo ni ongezeko la asilimia 10.2 mwaka hadi mwaka, na uwekezaji wake wa viwandani uliongezeka kwa asilimia 25.3, na kuonesha imani ya wajasiriamali katika siku zijazo.

Uwekezaji wa nje ya nchi pia unaendelea kuongezeka katika mji huo. Katika robo tatu za kwanza za Mwaka 2021, kulikuwa na miradi 76 yenye uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 10 za Kimarekani huko Dongguan, ikihusisha uwekezaji wa kigeni wa karibu dola bilioni 3.75 za Kimarekani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 111.5 mwaka hadi mwaka.

Dongguan imeweka nguvu kubwa katika kuchukua uvumbuzi wa sayansi na teknolojia kama injini yake ya kuendesha sekta yake ya viwanda, kuweka mpango mpya kabisa wa siku zijazo za mji huo "Kiwanda cha Dunia."

Mwaka 2021, sekta ya utengenezaji wa bidhaa za teknolojia ya juu mjini Dongguan iliendelezwa kwa haraka. Kwa mfano, thamani ya pato la bidhaa za roboti za viwandani iliongezeka kwa asilimia 66.8, saketi zilizounganishwa ziliongezeka kwa asilimia 22.5, na thamani ya uzalishaji wa magari yanayotumia nishati mpya iliongezeka kwa asilimia 62.5.

Kwa ujumla uwekezaji katika tasnia hiyo ya viwanda vya teknolojia ya kiwango cha juu uliongezeka kwa asilimia 26.2 mwaka hadi mwaka. Kwa sasa, kuna kampuni 7,387 za teknolojia ya juu za ngazi ya taifa huko Dongguan, na idadi bado inakua kwa karibu 1,000 kila mwaka katika miaka ya hivi karibuni.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha