Mapato ya Kifedha ya China yapanda kwa asilimia 10.7 Mwaka 2021

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 26, 2022

Xu Hongcai (Kulia), Naibu Waziri wa Fedha wa China akishiriki mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China kuhusu mapato na matumizi ya fedha ya China Mwaka 2021, mjini Beijing, Mji Mkuu wa China, Januari 25, 2022. (Xinhua/Pan Xu)

BEIJING - Xu Hongcai, Naibu Waziri wa Fedha wa China amesema Jumanne ya wiki hii kwamba, mapato ya kifedha ya China yalipanda kwa asilimia 10.7 mwaka hadi mwaka na kufikia Yuan trilioni 20.25 (sawa na dola trilioni 3.19 za Marekani) Mwaka 2021.

Xu amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, mapato ya kifedha ya China katika Mwaka 2021 yaliongezeka karibu mara mbili ikilinganishwa na mapato ya yuan trilioni 11.73 Mwaka 2012.

Ameeleza kwamba, Serikali Kuu ilikusanya mapato yapatayo yuan trilioni 9.15, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.5 mwaka hadi mwaka, huku serikali za mitaa zikishuhudia mapato yakiongezeka kwa asilimia 10.9 hadi yuan trilioni 11.1.

"Kufufuka kwa ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa kiwango cha bei ya wazalishaji kulisaidia mapato ya serikali kuu na serikali za mitaa kuongeza," Xu amesema.

Pato la Taifa la China (GDP) liliongezeka kwa asilimia 8.1 Mwaka 2021, na kupita lengo lililowekwa na serikali.

"Ukuaji tulivu wa Pato la Taifa umeweka msingi mzuri wa ukuaji wa mapato ya kifedha nchini," Xu amesema.

Hata hivyo, ukuaji wa mapato ya kifedha ulikuwa kwa wastani wa asilimia 3.1 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, chini ya wastani wa ukuaji wa Pato la Taifa wa asilimia 5.1 kwa kipindi cha miaka miwili. Xu ameonya kwamba, sehemu ya mapato ya kifedha katika Pato la Taifa iliendelea kushuka katika kipindi hicho, jambo ambalo linaonesha uungwaji mkono wa kifedha kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ulisalia chini ya shinikizo kubwa.

Xu amesema, mwaka huu China itachukua hatua madhubuti za kupunguza ada na ushuru ili kusaidia taasisi za soko na mchanganyiko wa sera zenye motisha.

Amesema, hatua hizo zitakuwa sahihi zaidi na endelevu ili kukidhi mahitaji ya taasisi za soko.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha